Marekani kufanya mazungumzo ya tatu na Iran juu ya nyuklia
25 Aprili 2025Marekani imetangaza kwamba ujumbe wake utakutana siku ya Jumamosi na maafisa wa Iran huko Oman kwa mazungumzo ya mara ya tatu juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Tammy Bruce amesema duru inayofuata itazikutanisha kwa mara ya kwanza timu za kiufundi. Michael Anton, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Sera ya Mipango ya Marekani ataongoza ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo hayo.
Soma zaidi:Iran yapendekeza mazungumzo ya nyuklia na nchi za Ulaya
Wiki iliyopita, mjumbe maalum wa Marekani katika mashariki ya kati Steve Witkoff aliongoza ujumbe wa Marekani mjini Roma walipokutana kwa mazungumzo ya mara ya pili na wajumbe wa Iran walioongozwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi na ambapo waliripoti kwamba mazungumzo yalikwenda vizuri.