Marekani yawawekea vikwazo viongozi wa Rwanda na M23
21 Februari 2025Jenerali mstaafu James Kabarebe pamoja na msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyuka na makampuni yake mawili yaliyoko ulaya wamewekewa vikwazo vya kiuchumi kwa shutuma za kuhusika katika machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kauli ya Rwanda imetolewa kupitia tangazo la msemaji wa serikali ya Rwanda kwa umma huku Rwanda ikisema vikwazo vya Marekani ambavyo vina lengo la kuiadhibu Rwanda haviwezi kuleta suluhu la mzozo huo wa muda mrefu. Rwanda imesema kupitia tangazo hilo kwamba inauchukulia uamuzi wa Maekani kama kuingilia kati na kupuuzia michakato inayoendelea ya nchi za kiafrika ya kuleta amani barani humo ukiwemo mzozo wa mashariki mwa DRC.
Tangazo hilo la serikali ya Rwanda limesema kwamba kwa muda wa miaka mitatu iliyopita eneo la mpaka wa Rwanda upande wa magharibi limekabiliwa na hali ya usalama mdogo.
UN ina wasiwasi na hatua ya kusonga mbele ya M23
Hii imesababishwa jeshi la serikali ya Kinshasa likisaidiwa na wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa kihutu wa FDLR, jeshi la Burundi, jeshi la jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, mamluki kutoka ulaya pamoja na wanamgambo waliopewa silaha na serikali ya Kinshasa maarufu kama wazalendo. Makundi hayo yote tangazo hili linasema yamechochea tu mzozo huu badala ya kuleta suluhu, lakini Marekani imeyafumbia macho.
Jean Batiste Gasominari ni mwanasheria kitaaluma lakini pia mchambuzi wa siasa za maziwa makuu, anasema hakuna matumaini vikwazo hivi kubadili hali ya mambo
Marekani, umoja wa mataifa na nchi za ulaya wameendelea kuilaumu Rwanda kulisaidia kundi la M23 ambalo limekuwa likiyashinda majeshi ya serikali ya Kinshasa na kuyatwaa maeneo mengi mashariki mwa nchi hiyo. Rwanda nayo imeendelea kushikilia msimamo wake kwamba haitoi msaada kwa kundi hilo. Kwa kutolewa vikwazo hivyo baadhi ya wananchi wana maoni mseto.
Vikwazo sio suluhusu ya mgogoro wa Kongo
Nadhani hii itawapa hamasa zaidi wapiganaji wa M23 ni sababu gani hasa inawafanya kupigana maana sasa wataanza kujiona kama wasiosikilizwa na mataifa makubwa kama Marekani ambayo walitegemea ingewasaidia kuishawishi serikali ya Kinshasa kuwasikiliza, sasa kwa sababu viongozi wao wanaanza kuwekewa vikwazo basi inawezekana wakaona sasa hawana jinsi isipokuwa tu kuendelea kupigana na pengine kuyachukua maeneo zaidi kitu ambacho huenda hakitasaidia lolote.
Tunaamini vikwazo hivi haviwezi kuleta suluhu la tatizo, isipokuwa tu mazungumzo ya kisiasa kati ya serikali ya Kinshasa na kundi la M23. Tunaamini pia Marekani inautambua vema mzozo huu lakini imeamua tu kutazama upande mmoja wa Rwanda na M23 na kuiacha serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo siku zote imekataa kufanya mazungumzo na kundi la M23.Nadhani Marekani kama nchi inapaswa kuacha kuegemea upande mmoja katika mzozo huu
Vita Kongo vyasababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi Burundi
Wakati haya yakiendelea kuna wasiwasi kwamba huenda nchi za ulaya nazo zikafuata mfano wa Marekani kwa sababu hadi sasa Uingereza na Ujerumani zimeshawahoji mabalozi wa Rwanda kuhusu mzozo wa mashariki mwa DRC. Kwa upande mwingine lakini Rwanda imeyajibu mataifa hayo kwa kuyataka kuachana na hayo na badala yake yasaidie kutafuta suluhu la mzozo huu. Kundi la M23 kwa muda wa mwezi mmoja na nusu uliopita limeiteka miji mikuu muhimu ya Goma Kivu ya Kaskazini na Bukavu Kivu ya Kusini pamoja na kuendelea kuyatwaa maeneo mengi huku wasiwasi ukitanda mzozo kubadilika na kuwa wa kanda nzima ikiwa mikakati madhubuti haitachukuliwa.
Marekani imesema imemuwekea vikwazo vya kiuchumi Jenerali mastaafu na mkuu wa zamani wa jeshi la Rwanda kwakuwa ndiye kiungo muhimu kwenye mawasiliano kati ya Rwanda na kundi hilo la M23, Marekani pia imemuwekea vikwazo vya kiuchumi msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyuka pamoja na makampuni yake mawili yalosajiliwa Uingereza na Ufaransa.