Marais wa DRC na Rwanda watoa wito wa usitishwaji mapigano
19 Machi 2025Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wamefanya mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana mjini Doha, Qatar hapo jana. Tshisekedi na Kagame wametoa wito wa usitishwaji wa mapigano wa mara moja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Taarifa ya pamoja iliyotolewa pamoja na Qatar, ambaye kiongozi wake ndiye aliyekuwa mpatanishi wa viongozi hao, imesema usitishwaji huo wa mapigano unastahili kufanyika mara moja na bila masharti yoyote.
Soma zaidi: M23 sasa yasema haitoshiriki mazungumzo ya amani Luanda
Ila haijawa wazi iwapo hilo litawapelekea wanamgambo wa M23 kutofanya mashambulizi zaidi ukizingatia kwamba kwa sasa wanadhibiti eneo kubwa la mashariki mwa Kongo kuliko wakati mwengine wowote. Kongo inaituhumu Rwanda kwa kutuma silaha na majeshi yake kuwaunga mkono wanamgambo hao, ambao mashambulizi yao yamelitumbukiza eneo la mashariki mwa Kongo katika mojawapo ya mzozo mbaya zaidi katika miongo kadhaa.