MAR DEL PLATA:Bush akumbana na maandamano ya upinzani
5 Novemba 2005Polisi wa kuzuia ghasia nchini Argentina wametumia gesi ya kutoa machozi ili kuvunja maandamano dhidi ya Marekani katika mji wa mapumziko Mar del Plata.Waandamanaji kwa mamia wamevunja madirisha ya maduka na wamewarushia polisi mabomu ya petroli.Dazeni kadhaa ya watu wametiwa ndani.Mapambano hayo yametokea umbali usio hata kilomita moja kutoka kule kulikofanywa Mkutano wa Kilele wa nchi za Bara Amerika.Wakati huo Rais George W.Bush wa Marekani alikuwa akikutana na viongozi wengine wa kanda hiyo.Kabla ya kutokea machafuko hayo,kulifanywa mkutano wa hadhra kwa amani dhidi ya Marekani kwenye uwanja wa mpira.Huko kiasi ya waandamanaji 40,000 walimsikiliza Rais Hugo Chavez wa Venezuela akiituhumu serikali ya Bush kuwa inafanya njama ya kuivamia nchi yake.Vile vile alitoa wito kwa viongozi wengine kulikataa pendekezo linalopigiwa debe na Bush la kuwa na Eneo Huru la Biashara la madola ya Bara Amerika.