Maporomoko ya udongo yaua watu 1,000 Darfur Sudan
2 Septemba 2025Janga hilo lilitokea Jumapili baada ya mvua kubwa kunyesha kwa siku kadhaa na kuathiri vibaya Kijiji cha Tarasin kilichoko eneo la Jebel Marra. Kundi la wanamgambo wa Sudan Liberation Movement (SLM) linaloongozwa na Abdulwahid al-Nur limesema hayo.
Kundi hilo limesema taarifa za awali zimedokeza kutokea vifo vya wakaazi wanaokadiriwa kuzidi 1,000 wote wa kijiji kimoja na kwamba mkaazi mmoja pekee ndiye amenusurika. SLM imetaja maporomoko hayo kuwa janga kubwa na lenye uharibifu mkubwa.
Kundi hilo limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada kusaidia juhudi za kutafuta watu au miili ambayo imenaswa kwenye udongo na vifusi.
Picha zilizochapishwa na SLM katika mitandao ya kijamii, zaonekana kuonyesha maeneo makubwa ya mlima yakiwa yameporomoka na kufunika kijiji kwa matope huku miti ikiwa imeng'olewa.
Jebel Marra ni eneo lenye safu ya volkano inayoenea umbali wa takriban kilomita 160 kusini-magharibi mwa mji mkuu uliozingirwa wa Darfur, Kaskazini ya El-Fasher, ambao wanamgambo wa RSF wanafanya mashambulizi kwa lengo la kuuteka baada ya kuuzingira kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Maporomoko ya ardhi yaliyotokea mwaka wa 2018 katika eneo jirani la Toukoli, yaliua takriban watu 20.
Gavana wa Darfur Minni Minnawi ameyataja maporomoko hayo kuwa janga la kibinadamu ambalo athari zake zinapita mipaka ya eneo hilo.
Kwenye taarifa, Minnawi ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada kuingilia kati kuwasaidia wahanga wa maafa hayo, akisema ni janga zito ambalo hawawezi kushughulia wao peke yao.
Janga hilo limejiri pia wakati wa majira ya mvua nchini Sudan, hali inayosababisha barabara nyingi za vijijini kutopitika.
Maashirika ya kimataifa ya misaada bado hayawezi kufika katika maeneo mengi ya Darfur, ikiwemo eneo lilikotokea maporomoko hayo, kwa sababu ya machafuko yanayoendelea kati ya wanamgambo wa RSF na jeshi la Sudan. Hali hiyo imekwamisha utoaji wa dharura wa misaada.
Sudan ilitumbukia kwenye vita vya kung'ang'ania mamlaka tangu Aprili 2023 kati ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anayeliongoza jeshi na aliyekuwa naibu wake, Kamanda Mohamed Hamdan Daglo, anayeongoza kundi la RSF.
Mapigano hayo yamesababisha umwagikaji mkubwa wa damu huku nchi hiyo ikikabiliwa na janga baya zaidi la kibinadamu ulimwenguni kote.
Makumi kwa maelfu ya watu wameuawa na mamilioni kuyapoteza makaazi yao.
Wanamgambo wa SLM hudhibiti sehemu za Jebel Marra lakini hawahusiki na machafuko ya sasa. Kutokana na hali hiyo maelfu kwa maelfu ya watu wamekimbilia usalama wao katika maeneo yanayodhibitiwa na SLM.
Kulinga na Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 10 ni wakimbizi kwa sasa nchini Sudan, na wengine milioni nne wamehamia nchi jirani.
(AFPE)