Mapigano yazuka Tripoli baada ya kuuawa kwa kamanda wa SSA
13 Mei 2025Kiongozi huyo Abdulghani Kikli, anayejulikana kwa jina maarufu la Ghaniwa, ni kamanda wa kikosi cha SSA, mojawapo ya makundi yenye nguvu ya kijeshi mjini Tripoli, lenye makao katika mtaa wenye wakaazi wengi wa Abu Salim.
Kundi hilo la SSA liko chini ya Baraza la Rais lililoingia madarakani mnamo mwaka 2021 pamoja na serikali ya kitaifa ya GNU ya Abdulhamid Dbeibah kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Miili 50 yagunduliwa kwenye makaburi ya pamoja, Libya
Wizara ya mambo ya ndani ya serikali ya kitaifa imetoa taarifa kwa umma ikiwahimiza kubaki majumbani kwa ajili ya usalama wao.
Kitengo cha Habari cha GNU kimesema mapema leo kwamba wizara ya ulinzi imechukua udhibiti kamili wa eneo la Abu Salim.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umetoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano mara moja na kurejesha utulivu, ikiwakumbusha jukumu lao la kuwalinda raia.