Mapigano yazuka tena mashariki mwa Kongo
12 Agosti 2025Haya ni kwa mujibu wa vyanzo vya kiusalama vilivyozungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP.
Kinshasa na waasi wa M23 walitia saini makubaliano mnamo Julai 19 ambapo walidhamiria usitishwaji wa kudumu wa mapigano.
Lakini makubaliano haya hayajasitisha mapigano kati ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na makundi ya kizalendo nchini humo yakihusisha silaha nzito nzito na wakati mwengine silaha ndogo ndogo.
Vyanzo nchini humo vinasema Jumapili pande zote mbili ziliviimarisha vikosi vyao.
Kufikia Jumatatu, mapigano bado yalikuwa yanaendelea katika eneo la Mulamba, mji ulio karibu kilomita 80 kusini magharibi mwa Bukavu, mji mkuu wa mkoa.
"Vikosi vyote vinatumia silaha nzito na mabomu yanarushwa kutoka kila sehemu huko Mulamba," alisema mkaazi mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP.
Tangu kuzuka kwake tena mwaka 2021, waasi wa M23 wamenyakua sehemu kubwa ya maeneo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikiwemo miji mikuu ya Goma mnamo Januari na Bukavu mwezi Februari.
Zaidi ya watu milioni 2 wameyakimbia mapigano hayo mashariki mwa nchi hiyo tangu Januari, kulingana na ripoti ya afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Kiutu iliyochapishwa mwishoni mwa mwezi Julai.