Mapigano yazidi Kivu Kusini, juhudi za amani zikiendelea
22 Agosti 2025Kuanzia Jumatatu hadi Jumatano, karibu watu wanane wamepoteza maisha katika mapigano yaliyotokea kwenye baadhi ya vijiji vya wilaya ya Mwenga, vinavyopakana na wilaya ya Uvira, hali iliyoongeza wasiwasi kwa wakaazi wa eneo hilo.
Mapigano kati ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda na jeshi la Kongo, linalosaidiwa na wapiganaji wa Wazalendo, yameripotiwa tangu mwanzoni mwa wiki, hasa katika vijiji vya Kizuka na Muhuzi vilivyoko wilaya ya Mwenga, kaskazini-magharibi mwa Uvira. Hali hii imezua taharuki, huku wakaazi wakihofia uwezekano wa mji wao kushambuliwa na waasi wa AFC/M23.
Viongozi wa mashirika ya kiraia wamekutana leo na wakazi wa Uvira kujadili hali ya usalama na kuangalia hatua za kuchukua ili kukabiliana na vitisho vya mashambulizi vinavyoendelea.
Waasi wa AFC/M23 wajipenyeza zaidi Uvira na Fizi
Kwa mujibu wa mashirika ya kiraia ya eneo hilo, waasi wa AFC/M23 wanajaribu kupenya kwenye maeneo ya Uvira na Fizi, lakini mara nyingi wanazuiliwa na jeshi la Kongo kwa msaada wa wapiganaji wa Wazalendo.
Mafikiri Masimango, mwanaharakati wa shirika la kiraia Uvira anawaonya raia kuendelea kuwa waangalifu.
Siku ya Jumatatu, mapigano mengine yaliripotiwa katika vijiji vya Kalungu na Kageregere, vilivyoko kati ya wilaya za Uvira na Mwenga. Jeshi la Kongo linasema liliweza kudhibiti shambulio hilo lililofanywa na waasi wa AFC/M23 kwa kushirikiana na wapiganaji wa kundi la Twirwaneho. Lilian, mkazi wa Uvira, anasema licha ya changamoto za kiusalama na kiuchumi, wakaazi bado wanajaribu kuendelea na maisha yao ya kila siku.
Katika taarifa tofauti, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa AFC/M23 wameendelea kushutumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano, kila upande ukiutuhumu mwingine kwa kuanzisha mashambulizi katika vijiji vya majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini. M23 imeonya kwamba haitasita kujibu mashambulizi yoyote dhidi ya ngome zake.
Mamlaka za mitaa huko Uvira zinakadiria kuwa zaidi ya familia 5,000 zimekimbia makazi yao na sasa zinakabiliwa na hali ngumu za maisha katika miji na vijiji vya eneo hilo.