Mapigano ya kimadhehebu yauwa 89 Syria
15 Julai 2025Takriban watu 89 wameuwawa katika mkoa wa Kusini mwa Syria wa Sweida kufuatia mapigano yaliyoingia siku ya pili leo Jumatatu, kati ya jamii ya Wasunni kutoka kabila la Mabedui na wapiganaji wa Kidruze.
Mapigano hayo ya kimadhehebu yanaonesha changamoto zinazomkabili kiongozi wa muda wa Syria Ahmad al Sharaa,katika nchi hiyo iliyoshuhudia vita kwa miaka 14.
Wakati vita hivyo vya kimadhehebu vikitanuka, Israel ambayo awali ilionya kwamba itaingilia kati nchini Syria kuwalinda Wadruze, imesema imefanya mashambulio katika eneo hilo la Sweida bila ya kutowa ufafanuzi zaidi.
Jeshi la Syria na wizara ya mambo ya ndani wametangaza kupelekwa kwa vikosi vya jeshi kuwalinda raia na kuahidi kudhibiti vita hivyo haraka na kwa ufanisi. Vita hivyo vilichochewa na tukio la kutekwa nyara muuza mboga mmoja wa Kidruze, na watu wenye silaha kutoka kabila la Mabedui.