Mapigano makali yazuka kati ya jeshi la Sudan na RSF
20 Mei 2025Jeshi la Sudan limesema operesheni yake ni ya kulisambaratisha kabisa kundi hilo, ambalo limekuwa likipamnana nalo tangu mwezi Aprili mwaka 2023. Msemaji wa jeshi, Nabil Abdallah, amesema katika taarifa yake kwamba, wapo katika operesheni kubwa na wananuia kuusafisha mji wa Khartoum kutokana na wanamgambo hao aliowaita majambazi.
Kulingana na muandishi habari wa shirika la AFP, mripuko mkubwa ulisikika katika eneo waliko RSF baada ya kupoteza udhibiti wa mji mkuu wa Sudan Khartoum mnamo mwezi Machi. Katika wiki za hivi karibuni kundi la RSF limekuwa likishambulia kwa kutumia droni katika maeneo tofauti ya nchi hasa katika mji wa Port Sudan yalipo makao makuu ya jeshi.
Shambulizi la kombora la RSF laua watu 14 Darfur
Mtaalamu wa Umoja wa Mtaifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, Radhouane Nouicer, amesema viwango vya mashambulizi hayo ya droni vinaonesha namna mgogoro huo unavyoendelea kutanuka na kutoa hatari kubwa kwa raia.
Ameongeza kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundo mbinu, yanayofanywa katika maeneo yaliyojaa watu, yanaweka maisha ya raia hatarini, kufanya hali ya kibinaadamu kuwa mbaya zaidi na kuhatarisha pia haki za msingi za binaadamu.
Kamil al-Taib Idris ateuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Sudan
Huku hayo yakiarifiwa, Jenerali Abdel Fatah al Burhan, amemteua waziri Mkuu wa kwanza wa Sudan tangu taifa hilo lilipoingia katika mapigano miaka miwili iliyopita. Kamil al-Taib Idris atakuwa na jukumu la kuunda serikali ya mpito, hatua ambayo imekuwa ikiungwa mkono na Burhan hasa baada ya jeshi kuchukua tena udhibiti wa mji wa Khartoum.
Waziri Mkuu aliyekuwepo Abdalla Hamdok alijiuzulu mwaka 2022 wakati wa mkwamo wa kisiasa na maandamano ya kudai demokrasia. Muandishi habari na mchambuzi wa kisiasa Osman Mirghani, amesema kuteuliwa kwa Idris ni hatua muhimu kuelekea kurejesha utawala wakiraia na kupata majibu ya mgogoro wa kisiasa wa Sudan. Amesema nafasi yake ya kukubalika na watu wa Sudan pamoja na wanamgambo wa RSF ni kubwa kutokana na Idris kutoegemea upande wowote wa kisiasa. Idris amewahi kufanya kazi kama mshauri wa masuala ya Sudan katika Umoja wa Mataifa na ni mwanachama wa kamisheni ya kimataifa ya sheria ya Umoja huo.
Mji wa Port Sudan washambuliwa kwa droni kwa siku ya sita
Vita vya Sudan vimeigawa nchi mara mbili, jeshi likiwa linadhibiti eneo la Kaskazini, Mashariki na Sudan ya Kati huku wanamgambo wa RSF wakidhibiti karibu eneo zima la Darfur na sehemu ya maeneo ya Kusini. Kando na vita hivyo kusababisha vifo vya maelfu ya watu pia mgogoro huo wa miaka miwili umesababisha watu wengine zaidi yamilioni 13 kukosa makazi huku zaidi ya milioni tatu wakiitoroka nchi.
Vita hivyo vimesababisha pia uchumi wa nchi kuanguka vibaya huku huduma za afya zikilemewa. Asilimia 90 ya hospitali zimefungwa kutokana na mapigano hayo huku wanawake na wasichana wakipitia mateso makubwa ikiwemo unyanyasaji wa kingono, kubakwa kwa makundi pamoja na mauaji yote haya yakidaiwa kufanywa na wanamgambo wa RSF hii ikiwa ni kulingana na ripoti za Umoja wa Mataifa.
afp/ap