Machafuko yazuka mkoa wa Kusini nchini Syria
15 Julai 2025Wizara ya mambo ya ndani ya Syria imesema vikosi vya usalama vya serikali vimeingia hivi leo katika mji huo wa Sweida unaokaliwa na idadi kubwa ya jamii ya Druze kwa lengo la kuyadhibiti machafuko yanayoihusisha jamii hiyo na wale wa makabila ya Kibedui.
Kufikia sasa, machafuko hayo yamesababisha vifo vya takribani watu 100 kufikia sasa. Ezzeldin Al- Shamaier ni kiongozi katika wizara ya ulinzi ya Syria na anasema hivi sasa dhamira yao kubwa ni kuyadhibiti magenge yanayosababisha vurugu na machafuko kwenye mji huo wa Sweida.
"Hivi sasa tumesimama pembezoni mwa kijiji cha Al-Mazra viungani mwa mji wa Sweida ambao unaoweza kuonekana nyuma yetu.Lengo letu ni kuwalinda wakaazi ikiwa hawatojiingiza kwenye mapambano dhidi ya vikosi vya usalama vya serikali. Lengo letu la msingi ni kuwalinda raia dhidi ya magenge ambayo yanasababisha vurugu na taharuki katika mji.''
Usitishaji mapigano
Muda mfupi baada ya jeshi kuingia Sweida, wizara ya ulinzi ya Syria ikatangaza usitishaji mapigano. Kwa muda mji wa Sweida umekuwa ukidhibitiwa na makundi yenye silaha kutoka jamii ya Wadruze ambao viongozi wao wa kidini wanasema waliidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wa serikali na kuwatolea pia mwito makundi hayo ya wapiganaji kuweka chini silaha.
Lakini baada ya mwito huo kiongozi mmoja wa kidini mwenye ushawishi mkubwa kwenye jamii hiyo, Sheikh Hikmar al-Hijri ,ambaye imeelezwa mwanzoni aliridhia kuhusu hatua ya vikosi vya serikali kuingia Sweida, alibadili mtazamo na kutowa taarifa baadae ya kuyataka makundi hayo kupambana kuzuia kampeni yoyote ya ukatili kwa njia zote.
Kiongozi huyo hataki uingiliaji kati wa jeshi la serikali na badala yake anataka jeshi la kimataifa kuingia Sweida.
Jeshi la Syria lapingwa na Mabedouin
Jeshi la serikali limesema limeingia kwenye mji huo kutenganisha pande mbili zinazopigana lakini wameishia kuchukuwa udhibiti wa maeneo mengi yaliyokuwa yakikaliwa na jamii ya Wadruze kwa mujibu wa mwandishi habari wa AFP.
Mwandishi huyo ameripoti kwamba wanajeshi chungunzima wameonekana wakielekea Sweida leo asubuhi huku silaha nzitonzito zikipelekwa karibu na mji huo.Tangu Jumapili yalipozuka machafuko watu 99 wakiwemo wanajeshi 18 wameuwawa.
Wadruze wanadai jamii ya Mabedui wanashirikiana na wanajeshi wa serikali ya Syriakuwaandama.
Kwa upande mwingine Israel imejitokeza ikijinadi kuwa mtetezi wa Wadruze nchini Syria na ikiwaona kama jamii inayoweza kuwa washirika wake.
Shirika la habari la Syria limesema kwamba jeshi la Israel limefanya mashambulizi ya anga kwenye mji wa Sweida, hii ikifuatiwa na onyo la hapo jana la Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, dhidi ya jeshi la serikali ya Syria kuwaandama watu wa jamii ya Druze.