Rwanda kuzishitaki Burundi, DRC na Ubelgiji
10 Aprili 2025Kauli hii imetolewa katika mkesha wa usiku wa kumbukumbu za mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi wa Rwanda mwaka 1994, ambapo manusura wametoa ushuhuda uliotoa picha ya mauaji mabaya, walionusurika miaka 31 iliyopita. Ni mkesha ambao umefanyika katika ukumbi wa BK Arena mjini Kigali ambao kwa kawaida unabeba watu elfu tano na ulifurika umati wa waombolezaji.
Ni usiku uliotawaliwa na simanzi, machozi na shuhuda za kusisimua mara kadhaa waombolezaji waliangaa vilio vya hapa na pale kutokana na mkanganyiko uliosababishwa na kumbukumbu hizo
Kagame azilaani nchi zinazoiwekea Rwanda vikwazo
Manusura wakatoa shuhuda za kusisimua. Bi Lilian Murangwayire ambaye mwaka 1994 alikuwa na umri wa miaka 14 tu amesema katika familia ya watu 12 alinusurika yeye na dada zake wawili wadogo.
“Tarehe 13 mwezi wa nne mwaka 1994 tuliamua kukimbilia katika kanisa katoliki la Ntarama, hapa tulidhani hawawezi kutuua tukiwa katika nyumba ya Mungu, kulikuwepo idadi kubwa ya wakimbizi wa kitutsi waliokuwa wamekimbilia hapo lakini siku moja baadaye yaani tarehe 15, walikuja interahamwe na wanajeshi wa serikali walitumia mapanga, shoka, sime, mawe makubwa, jembe, mikuki na kila aina ya silaha ya jadi walitumia na kutuangamiza. Mimi nilikatwakatwa sehemu nyingi na mwisho kupoteza fahamu, waliondoka wakidhani mimi pia nilikuwa nimekufa lakini kumbe nilibaki hai," alisema Bi Murangwayire.
Baada ya mauaji wanamgambo wa kihutu walikimbilia DRC
Baada ya kusimamisha mauaji hayo mwezi wa saba mwaka 1994 wanamgambo wa kihutu wa Interahamwe na wanajeshi wa serikali ya zamani nchini Rwanda wengi walikimbilia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwisho kuunda kundi la wapiganaji wa FDLR ambao hadi hii leo wananuia kuing’oa madarakani serikali ya Rwanda kutokea mashariki mwa Congo.
Shirikisho la mashirika ya manusura wa mauaji hayo IBUKA limesema kwamba kwa sasa wapiganaji hao licha ya kupewa hifadhi na nchi ya Kongo kwa miaka 31 iliyopita, sasa hivi nchi za Kongo, Burundi na Ubelgiji zimeonyesha wazi kuliunga mkono kundi hilo lenye itikadi ya ubaguzi na msimamo mkali wa mauaji kwa misingi ya ukabila
Kagame: Tutalinda usalama wa Rwanda kwa gharama yoyote
wapiganaji wa FDLR wadaiwa kueneza itikadi zenye msimamo mkali
Mwenyekiti wa shirikisho la mashirika ya manusura wa mauaji ya Rwanda Dr Phillibert Gakwenzire akaiomba serikali ya Rwanda kutolifumbia macho suala hilo na badala yake ipeleke shitaka dhidi ya nchi hizo katika mahakama za kimataifa kwa ajili ya haki za binadamu.
“Katika kueneza itikadi ya mauaji ya kimbari, chuki na kubeza na kukanusha mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi,kundi la FDLR kwa sasa linasaidiwa na mataifa kadhaa, ikiwa ni pamoja na jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Burundi pamoja na Ubelgiji, shirikisho letu linaiomba serikali kuyashitaki mataifa haya katika mahakama za kimataifa kwa sababu vitendo hivi hatuwezi kuvivumilia tena,’’ alisema Dr Phillibert Gakwenzire.
Manusura wanasema wakati umoja na maridhiano ukiendelea vizuri nchini Rwanda upande wa pili wapiganaji hawa wa FDLR kwa misaada ya nchi hizo wameendelea kueneza itikadi zenye msimamo mkali na washirika wake hasa kupitia mitandao ya kijamii huku wakipotosha historia ya kutokea kwa mauaji hayo.
Kundi la FDLR limekuwa mwiba mkali katika uhusiano kati ya Rwanda na Kongo na kwa kuwa kila nchi inaishutumu mwenzie kuwasaidia maadui zake. Lakini tangu kuzuka kwa vita mashariki mwa Kongo pia Burundi na Rwanda zimejikuta katika wakati mgumu na sasa Ubelgiji nayo hali imekuwa mbaya zaidi.