Mamia ya waumini wazuru kaburi la Papa Francis
27 Aprili 2025Waombolezaji wengi wamepita kwenye kaburi hilo huku wakifanya ishara ya msalaba au kupiga picha kwenye simu zao.
Wahudumu waliongoza foleni ya maelfu waliomiminika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma kuliona kaburi hilo.
"Papa Francis alinipa hamasa kubwa, alikuwa mwongozo kwangu,” amesema Elias Caravalhal.
Soma pia: Papa Francis azikwa mjini Roma
Caravalhal anaishi mjini Roma lakini hakufanikiwa kutoa heshima zake za mwisho kwa Papa Francis wakati mwili wake ulipolazwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro baada ya kifo chake mnamo siku ya Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88.
Caravalhal amesema amelitembelea kaburi la Papa ili kumshukuru kwa yote aliyoyafanya.
Waridi jeupe limewekwa juu ya kaburi lake lililoandikwa "Franciscus” ambalo ni jina la Papa huyo kwa lugha ya Kilatini.
Misa ya mazishi ya Papa yahudhuriwa na maelfu ya watu
Kaburi hilo limefunguliwa kwa siku ya pili kati ya siku tisa za maombolezo rasmi, na baada ya hapo kutafanyika mkutano maalum wa kumchagua papa mpya.
Misa maalum pia iliandaliwa na Kadinali Pietro Parolin katika uwanja wa mtakatifu Petro. Parolin anachukuliwa kama mmoja wa watu wanaoweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya kutokana na nafasi yake ya juu katika uongozi wa Kanisa Katoliki.
"Mchungaji ambaye Bwana aliwapa watu wake, Papa Francis, ameimaliza safari yake duniani na ametuacha,” Parolin alisema katika misa iliyofanyika Jumapili ambayo ilikuwa ya kwanza baada ya Pasaka.
Soma pia: Vurugu zashuhudiwa Vatican watu wakiendelea kumuaga Papa
"Huzuni ya kuondoka kwake, hisia za masikitiko zinazotuandama, maumivu moyoni mwetu, hali ya kuchanganyikiwa: tunapitia yote hayo kama walivyozuhunika watu wakati wa kifo cha Yesu.”
Misa hiyo imehudhuriwa na umati wa watu unaokadiriwa kuwa 200,000 wakiwemo vijana wengi waliokwenda Roma kwa ajili ya kutangazwa mtakatifu kwa kijana wa kwanza wa milenia, Carlo Acutis, katika siku maalum zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya vijana.
Makundi ya vijana, baadhi wakiwa wamevalia sare za skauti, walihudhuria mazishi ya Papa Francis siku ya Jumamosi na wameujaza uwanja wa Mtakatifu Petro leo Jumapili.
Hakuna tarehe maalum iliyowekwa kwa ajili ya mkutano wa kumchagua papa mpya lakini unatarajiwa kufanyika kati ya Mei 5 na 10. Makadinali waliokwenda Roma kwa ajili ya mazishi ya Papa Francis watakuwa na mikutano ya mara kwa mara wiki hii kujadili mustakabali wa Kanisa Katoliki lenye waumini bilioni 1.4 kote duniani.
Soma pia: Waafrika wana matamanio ya Papa kutoka kwao
Papa Francis alichagua mahali pa kuzikwa katika kanisa Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore badala ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro huko Vatican walikozikwa watangulizi wake wengi, kwa sababu sehemu hiyo inaakisi maisha yake ya "unyenyekevu, na ya kawaida,” alisema askofu mkuu anayesimamia Kanisa hilo Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore.
"Ni vigumu kuamini kwamba hayupo tena nasi,” amesema Susmidah Murphy, mtalii kutoka Kerela, India.
"Ni huzuni mkubwa kwa sababu hatupati mapapa wa aina hii mara kwa mara.”