Mamia waandamana Gaza kupinga vita na uongozi wa Hamas
26 Machi 2025Waandamanaji wa Kipalestina walioonekana katika moja ya machapisho ya mtandao wa kijamii wa X wamesikika wakisema kundi la Hamas linapaswa kuondoka madarakani. Video kadhaa na picha zinaashiria maandamano hayo yamefanyika Machi 25 huko Beit Lahiya kaskazini mwa Gaza.
Eneo hilo la kaskazini mwa ukanda huo ni moja ya sehemu zilizoathiriwa vibaya katika vita kati ya Israel na kundi la Hamas. Majengo mengi katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu yamesambaratishwa wakati wakaazi wamelazimika kuhama mara kadhaa kuepuka mzozo.
Maelfu ya wakaazi waliolazimika kukimbilia kusini mwa Gaza mwanzoni mwa vita hivyo ambavyo vimeshawauwa zaidi ya Wapalestina 50,000kulingana na mamlaka za Ukanda huo, walirejea mwezi Januari baada ya makubaliano ya kusitisha vita kuanza kutekelezwa. Hata hivyo, Isael ilianzisha tena mashambulizi mapya Machi 18 na kufifisha matumaini ya vita kukoma katika Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Mahmoud Abbas ataja kuwa tayari kuiongoza Gaza baada ya vita
Hayo yanaendelea wakati Umoja wa Mataifa ukipunguza theluthi moja ya wafanyakazi wake wa kimataifa katika Ukanda wa Gaza. Mmoja wa wasemaji wa Umoja wa Mataifa Alessandra Velluci, amebainisha kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres hawezi kuwahakikishia wafanyakazi hao usalama wao.
Miongoni mwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yatakayoathiriwa na kupunguzwa kwa wafanyakazi wake Gaza ni pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula, WFP, Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la kuhudumia watoto UNICEF.
Muongoza filamu wa Kipalestina aliyekamatwa aachiliwa huru
Katika hatua nyingine, mamlaka za Israel zimemwachilia huru muongoza filamu wa Kipalestina aliyeshinda tuzo za Oscar katika filamu yake ya "No Land," Hamdan Ballal sambamba na Wapalestina wengine wawili. Ballal na wenzake walikamatwa kwa tuhuma za kuwarushia mawe walowezi wa Kiyahudi. Kabla ya kukamatwa na wanajeshi wa Israel Ballal anaripotiwa kuwa alipigwa.
Akilizungumzia tukio hilo baada ya kuachiliwa huru Ballal amesema, ''Lilikuwa shambulio kali na lengo lilikuwa kuua. Baada ya kushinda tuzo ya Oscar sikutarajia kuwa kwenye hatari ya mashambuliz ya aina hii.''
Kulingana na wizara ya afya ya Palestina, wanajeshi wa Israel wameshawauwa Wapalestina 913 katika Ukingo wa Magharibi wakiwemo wanamgambo.