Maafisa wastaafu Israel wahimiza kusitisha vita Gaza
4 Agosti 2025Maafisa hao wa zamani wameutoa wito huko katika barua ya wazi iliyosambazwa na vyombo vya habari mapema leo Jumatatu wakieleza kuwa uamuzi wao wa kitaalamu unaonyesha kwamba Hamas si tishio tena la kimkakati kwa Israel.
Barua hiyo imetiwa saini na watu wapatao 550, wakiwemo wakuu wa zamani wa idara ya usalama wa ndani (Shin Bet) na shirika la kijasusi la Mossad, imemtaka Trump "kumpa mwongozo" Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu namna ya kuelekea kwenye usitishaji mapigano. Wakuu watatu wa zamani wa Mossad Tamir Pardo, Efraim Halevy na Danny Yatom ni miongoni mwa waliotia saini barua hiyo.
Ami Ayalon, mkurugenzi wa zamani wa idara ya usalama wa ndani Shin Bet amesema mwanzoni vita hivi vilikuwa vita vya haki, vita vya kujihami, lakini Israel ilipofikia malengo yote ya kijeshi, sasa vita hivi si vita vya haki tena. Ayalon ameendelea kwa kutahadharisha kuwa vita hivyo vinavyokaribia mwezi wa 23, vinapelekea Taifa la Israel kupoteza usalama na utambulisho wake.
Yaliyomo kwenye barua, msimamo wa Netanyahu
Barua hiyo imeweka wazi kuwa kwa muda mrefu sasa, jeshi la Israel limetimiza malengo mawili ambayo yalitakiwa kufikiwa kwa nguvu, nayo ni kuisambaratisha Hamas kijeshi na kiutawala. Na kwamba lengo la tatu na muhimu zaidi, linaweza kupatikana tu kupitia makubaliano na kuwarejesha mateka wote nyumbani, huku ikisisitiza kuwa maafisa wakuu waliosalia wa Hamas wanaweza kuendelea kusakwa baadaye.
Barua hiyo imetolewa wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwa atalitokomeza kabisa Kundi la Hamas na kuwakomboa mateka wote huku akilituhumu kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina kutokuwa na nia ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano wala kuwaachilia mateka kwa kuwa wanawatesa mateka kama walivofanya manazi wa Ujerumani kwa wayahudi.
" Na ninapoona hili, ninaelewa kile ambacho Hamas wanataka. Hawataki makubaliano, wanataka kutuvunja moyo na video hizi za kutisha, kupitia propaganda za uwongo wanazoeneza ulimwenguni. Lakini hatutavunjika moyo. Nina ari zaidi ya kuwakomboa mateka wetu, kuiondoa Hamas, ili kuhakikisha kwamba Gaza haitokuwa tena tishio kwa taifa la Israel."
Hapo jana, Netanyahu alitoa wito kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC kuwasaidia mateka waliopo Gaza kwa kuwapatia chakula na matibabu ya haraka, baada ya Hamas kusambaza video zinazoonyesha mateka wawili wakiwa wamedhoofika.
Danny Danon, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya kikao cha dharura kuhusu hali ya mateka wa Israel huko Gaza, baada ya ukosoaji mkubwa kufuatia video iliyosambazwa na Hamas.
//AP, DPA, Reuters, AFP