Mameya watatu wa vyama vya upinzani Uturuki wakamatwa
5 Julai 2025Maafisa wa chama kikuu cha upinzani CHP wamitaja hatua hiyo kuwa ni "operesheni ya kisiasa" inayolenga kuwakandamiza viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.
Mameya hao kutoka miji ya Adana, Antalya na Adiyaman—walikamatwa kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ufisadi, ambao pia ulimhusisha meya wa zamani wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, aliyefungwa jela mwezi Machi. Imamoglu, ambaye ni mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan, ndiye mgombea wa urais wa CHP kwa uchaguzi wa mwaka 2028.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, mameya wa Adana na Adiyaman wanahusishwa na kesi ya kupanga zabuni na rushwa, iliyoanzishwa na ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma wa Istanbul. Meya wa Antalya, kwa upande wake, anakabiliwa na uchunguzi tofauti kuhusu tuhuma za rushwa, ambapo pia mwanawe alikamatwa.
Mapema wiki hii, polisi waliwakamata watu zaidi ya 120 katika mji waIzmir, ngome ya upinzani, kwa tuhuma zinazohusiana na ufisadi.