Malori zaidi ya misaada yaendelea kuingia Gaza
28 Julai 2025Takriban malori 120 yaliyosheheni chakula na vifaa vingine yameingia Gaza na mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameanza usambazaji wa misaada hiyo kwa Wapalestina waliokuwa wakikabiliwa na njaa. Hayo yameelezwa na idara iliyo chini ya wizara ya ulinzi ya Israel ambayo inasimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina (COGAT) iliyoongeza kuwa malori mengine 180 yako tayari kuruhusiwa kuingia Gaza.
Kando na malori hayo, mataifa ya Israel, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu yamedondosha misaada ya chakula kwa kutumia ndege. Kabla ya kuanza kwa vita hivi kati ya Israel na Hamas vilivyodumu kwa miezi 21 huko Gaza, kulihitajika karibu malori 500 kwa siku ili kukidhi mahitaji ya Wapalestina wapatao milioni mbili.
Siku ya Jumapili, jeshi la Israel lilianza kutekeleza mpango wa usitishaji mapigano kwa muda wa saa kumi kwa siku katika maeneo matatu ya Gaza City, Deir al Balah na Mawasi, maeneo yenye idadi kubwa ya wakaazi, kama sehemu ya mfululizo wa hatua zilizoanzishwa ili kuongeza misaada ya kibinadamu kufuatia wasiwasi na ukosoaji wa kimataifa kwamba Israel inasababisha ongezeko la baa la njaa huko Gaza. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekanusha vikali tuhuma hizo.
"Israel inatajwa kuwa tunatumia kampeni ya njaa huko Gaza, ni uwongo mtupu. Hakuna sera ya njaa na wala hakuna njaa huko Gaza. Tunawezesha misaada ya kibinadamu kuingia Gaza katika muda wote wa vita."
Hatua za Israel zapongezwa na kukosolewa
Mkuu wa ofisi ya masuala ya kiutu na misaada wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher amepongeza hatua ya Israel kuruhusu uwepo wa njia salama kwa misafara ya kibinadamu inayoelekea Gaza , na kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utajaribu kadri ya uwezo wake kuwafikia watu wengi zaidi wanaokabiliwa na njaa katika ardhi ya Palestina.
Akiuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka jumuiya ya kimataifa kutoruhusu njaa kutumiwa kama silaha ya vita, akiongeza kuwa migogoro inaendelea kueneza njaa ambayo inachochea ukosefu wa utulivu na kudhoofisha juhudi za amani.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linawaleta pamoja viongozi wa ngazi za juu kujadili suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina. Mkutano huo wa siku mbili unaanza leo na utaongozwa na mataifa ya Ufaransa na Saudi Arabia lakini Israel na mshirika wake Marekani wametangaza kuususia.
(Vyanzo: AP, Reuters, DPA, AFP)