Malori mawili ya mafuta ya Dizeli yatarajiwa kuingia Gaza
3 Agosti 2025Shirika la habari la Al Qahera News lenye mafungamano na serikali ya Misri limeripoti leo kwamba malori mawili ya mafuta yaliyobeba tani 107 za dizeli yanatarajiwa kuingia Gaza, miezi kadhaa baada ya Israel kuweka vizuizi vya kuingiza bidhaa na misaada mengine katika ukanda huo wa Gaza.
Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema uhaba wa mafuta unakwamisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali hospitali.
Hata hivyo hakukuwa na uthibitisho iwapo malori hayo ya mafuta yamefanikiwa kuingia Gaza.
Kuanzia mwezi Machi, uingizwaji wa mafuta na misaada mengine ndani ya Gaza imekuwa nadra baada ya Israel kuweka vikwazo kama sehemu ya kuishinikiza Hamas kuwaachilia mateka waliobaki.
Wizara ya afya ya Gaza imeeleza kwamba watu kadhaa wamefariki kutokana na utapiamlo katika wiki za hivi karibuni. Jana Jumamosi, wizara hiyo ilitangaza vifo vya watu wengine saba, akiwemo mtoto mmoja.