Malaki waandamana Israel kutaka vita visitishwe Gaza
18 Agosti 2025Mji wa Tel Aviv ulio kitovu cha biashara nchini Israel, ndio ulishuhudia idadi kubwa ya watu mitaani usiku wa kuamkia Jumatatu waliojitokeza kuitaka serikali ya taifa hilo ikomeshe vita vya Ukanda wa Gaza na kuonesha mshikamano na mateka wanaendelea kuzuiliwa na wanamgambo wa Hamas.
Waandamanaji wapatao laki 2 waliingia mitaani wakipiga mayowe wakisema "Warejesheni mateka nyumbani! na Komeshani vita" na baadae kukusanyika kwa wingi kwenye eneo la wazi linalofahamika kama "Uwanja wa Mateka" katikati mwa Tel Aviv.
Kwenye miji mingine ya Israel kama ilivyokuwa kwa Tel Aviv waandamanaji walizifunga barabara muhimu.
Wengi walikuwa wamebeba bendera za taifa hilo za rangi nyeupe na buluu pamoja na zile za rangi ya manjano za kuonesha mshikamano na mateka.
Inaelezwa hayo ni miongoni mwa maandamano makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu kuanza kwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas mnamo Oktoba 2023.
Waandamanaji wasema wamechoshwa na vita vya Gaza
Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha idadi kubwa ya Waisraeli wamechoshwa na vita vya Gaza na wanaunga mkono kumalizwa vita hivyo kwa lengo la kuachiwa huru mateka walisalia. Inakadiriwa takribani mateka 50 wanazuiwa Gaza ikiwemo walio hao pamoja na miili ya waliouawa.
Mama wa mmoja wa mateka hao aliyeshiriki maandamano ya jana usiku amesema, "Tumechoshwa na vita, tumechoshwa na kutengwa, tumechoshwa na kujitoa kwetu sadaka, tumechoka na kusubiri ruhusa ya kutangaza mauaji ya mwanajeshi, tunataka makubaliano madhubuti yatakayowarejesha nyumbani mateka 50".
Rais Isaac Herzog wa Israel alikwenda kwenye uwanja uliofurika waandamanaji na kutoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa kundi la Hamas kuwaachia huru mateka.
Netanyahu na washirika wake walaani maandamano
Hata hivyo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wake wa fedha anayefahamika kwa misimamo mikali Bezalel Smotrich wameyalaani vikali maandamano hayo.
Kwenye ujumbe wake wakati wa kikao cha baraza la mawaziri, Netanyahu amesema wale wanaoshinikiza vita visitishwe hivi sasa bila kulishinda kundi la Hamas, wanaliongezea nguvu kundi hilo na kuteteresha uwezekano wa kuachiwa mateka.
Matamshi karibu sawa na hayo yametolewa na Smotrich aliyewatuhumu waandamanaji kwa "kampeni mbaya na ya hatari inayowaenga enga wanamgambo wa Hamas".
Maandamano hayo yametokea zaidi ya wiki moja baada ya baraza la usalama la Israel kuidhinisha mipango ya kuukamata mji mkubwa ndani ya Ukanda wa Gaza licha ya ukosoaji wa kimataifa kwamba mpango huo utazidisha masaibu na mateso kwa Wapalestina.