Je, makundi yanayomiliki silaha Myanmar yamedhoofika?
25 Julai 2025Ripoti ya mwezi Julai iliyochapishwa na shirika la utafiti la Marekani "Armed Conflict Location & Event Data" (ACLED) imesema Jeshi la Myanmar limo kwenye hatua za kasi na linakaribia kuliziba pengo la matumizi hayo ya droni.
Ripoti hiyo imeangazia zaidi matumizi ya droni kwa pande zote zinazopigana na taswira ya mashambulizi hayo katika vita vya nchini Myanmar.
Ingawa pande zote zinaendelea kutengeneza na kuimarisha droni, ripoti hiyo imebainisha kwamba mwaka 2025 unaonyesha wazi kwamba jeshi linazidi kujiimarisha.
Mwandishi wa ripoti hiyo Su Mon Thant ameiambia DW kwamba vikosi vinavyohusika na ndege zisizo na rubani vya upande wa upinzani haviwezi kufananishwa na rasilimali za jeshi la serikali ya Myanmar inayosaidiwa na China, kusalia mamlakani.
Amesema upinzani hauwezi kushindana na jeshi hata kidogo. Jeshi lina fedha, lina uwezo wa kuagiza maelfu ya droni kutoka China, kwa wakati mmoja wakati ambapo makundi ya upinzani, mara nyingine huhangaika hata kwa miezi mitatu kutafuta fedha za kununua angalau droni mbili tu.
Upinzani uliongezeka kwenye vita vya droni
Su Mon Thant amesema makundi ya upinzani yaliwahi kuongoza huko nyuma katika vita vya droni kwa usaidizi wa vijana wenyeji ambao walijikusanya kwenye maeneo ya mpakani mwa nchi na kuunganisha nguvu na majeshi ya waasi wa kikabila ambao tayari walikuwa wamejipanga huko.
Makundi hayo yalijifunza kwa kuangalia video zilizochapishwa kwenye ukurasa wa YouTube za vita vya nchini Ukraine, wakiangalia namna ya kutumia droni za kibiashara kwa ajili ya upelelezi na kuzibadilisha kuwa silaha za mauaji au kuunda zao wenyewe kwa kutumia plastiki, mbao na vifaa chakavu vya kielektroniki.
Droni zimekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya vikundi vya upinzani, hii ikiwa ni kulingana na Profesa wa Chuo cha Kitaifa cha masuala ya Vita, Zachary Abuza, aliyeko huko Washington, Marekani. Yeye pia amejikita katika masomo yanayohusu uasi kwenye eneo la Kusini mashariki mwa Asia.
Ameiambia DW kwamba makundi hayo yalikuwa na ubunifu mkubwa, yakianza kwa kufanya kama majaribio ya droni, lakini baadaye yakaongeza ufundi wa wanafunzi wenye ujuzi wa teknolojia waliokwenda msituni na kushirikiana na makundi hayo ama EROs. Akasisitiza kwamba "Huu ndio mwelekeo wa vita."
Abuza amesema hivi sasa kila kundi la upinzani nchini humo lina kikosi chake cha droni.
Kaskazini mwa Myanmar, kwenye jimbo la Karenni linalopakana na Thailand, kuna kikosi cha droni cha Karenni cha jeshi la Kitaifa kinachoongozwa na mhandisi wa teknolojia mwenye miaka 27 anayejiita 3D. Anajiita hivyo kutokana na utaalamu wake wa mashine ya kuchapa ama printer inayotumia teknolojia ya 3D.
3D, aliyekataa kutambulishwa kwa sababu za kiusalama, ameeleza kwamba timu yake yenye karibu watu 60 hutumia droni mara nyingi wanapokabiliana na makundi yanayopambana na jeshi.
Hutumia kwa ajili ya upelelezi, kushambulia ama kufikia maeneo wanayoyalenga. Amesema droni hizo wanazoziita kamikaze huwagharimu kiasi kidogo tu cha dola kununua.
Maendeleo ya teknolojia
Wachambuzi aidha wanasema hatua ya jeshi kuziongezea droni kamera maalumu zinazowawezesha kuchunguza hata kupitia kwenye kuta na usiku, pia kumefanya mashambulizi yake ya droni kufanikiwa zaidi.
Juu ya hayo, kufuatia ombi la serikali ya Myanmar mwaka uliopita, Beijing ilianza kuzuia mauzo ya vifaa vinavyoweza kutumiwa na mataifa hayo mawili ambavyo ni pamoja na droni, hali iliyoongeza ugumu kwa makundi ya upinzani kununua kwa kuwa pia vilikuwa ni ghali.
Lakini Abuza anasema makundi hayo sasa yameanza kutafuta namna ya kukabiliana na kikwazo hicho, kwa mfano kwa kununua baadhi ya vifaa badala ya droni ambayo tayari imeundwa, lakini pia wakiangazia maeneo mengine, zaidi ya China ambayo ndio mzalishaji wao mkubwa hadi sasa.
Kulingana na ripoti ya ACLED, ingawa makundi hayo ya upinzani yaliongeza sana mashambulizi ya droni tangu wakati wa mapinduzi nchini Myanmar, lakini yalianza kupungua kwa kasi tangu mwaka 2024, baada tu ya jeshi nalo kuanza kushambulia kwa kiasi kikubwa kwa kutumia droni.
Kulingana na kundi hilo la kitafiti, makundi hayo yalifanya mashambulizi 130 ya droni mnamo Januari 2024, na kila eneo lililolengwa lilikabiliwa na mashabulizi zaidi ya moja, lakini hali ilishuhudiwa kuanza kubadilika mnamo Februari 2025.
Lakini Su Mon Thant amesema mashambulizi ya droni huenda yasibadilishe mwelekeo wa vita hivyo lakini akatilia msisitizo kwamba jeshi linazitumia mara kwa mara kusaidia kuyadhoofisha mapigano na hata kuwalazimisha wapiganaji kurudi nyuma.
Lakini kwenye mahojiano hayo na DW, wapiganaji hao walisema mashambulizi ya droni yanayofanywa na jeshi huwaua wengi wao kuliko hata inavyotangazwa na vyombo vya habari vya Myanmar. Kulingana na ACLED,droni zimewaua karibu watu 80,000.