Makubaliano ya mkataba wa plastiki yagonga mwamba
15 Agosti 2025Mazungumzo kuhusu rasimu ya mkataba huo wa kuzuia matumizi ya plastiki yamemalizika bila kujua hatua itakayofuata kutokana mgawanyiko mkali baina ya wajumbe waliokuwa wanawakilisha nchi zaidi ya 180 katika mazungumzo hayo.
Ilitarajiwa kuwa angalau siku ya leo ijumaa rasimu ya awali ambayo ilikuwa imeandaliwa ili kuungwa mkono wa wajumbe wa mkutano wa wakilishi hao ingepitishwa, lakini mwishowe ilishindikana.
Mazungumzo ya Mkataba wa Plastiki yakwama Geneva
Zaidi ya wajumbe 100 wa vuguvugu la utashi kutoka Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Amerika Kusini, Afrika na Asia, waliazimia kukomesha mara moja matumizi ya plastiki katika vyombo vya kawaida vya matumizi ya nyumbani kama vile vikombe, sahani na vifaa vingine huku wakikazia plastiki zinazoweza kutumiwa tena lakini hawakufanikiwa.
Nchi zenye kuzalisha mafuta zikiwemo Saudi Arabia, Iran na hata Urusi, ambazo zinajiita kundi lenye maono sawa zenyewe zimeweka mkazo kuhusu kudhibiti takataka zitokanazo na plastiki badala ya kupunguza uzalishaji wake. Wataalamu wanasema plastiki hii inatokana na ukweli kwamba inalizishwa kutokana na mafuta kwa hiyo huenda nchi hizo zikawa zinazingatia suala la uchumi wake.
Ufaransa yasikitishwa na matokeo ya mkutano huo
Wajumbe katika mazungumzo haya walipania kupata mafanikio ya kupitisha rasimu hiyo lakini wakashindwa. Waziri wa mazingira nchini Ufaransa Agnes Pannier-Runacher ametangazwa kusikitishwa na matokeo ya mazungumzo hayo
"Baada ya siku kumi za majadiliano nimekata tamaa na nimechukia. Nimekata tamaa kwamba hatukuweza kufikia matarajio ya raia wetu kuhusu tishio linalosababishwa na athari za matumizi plastic kwa maisha yao na mazingira kwa ujumla. Na nimechukia kwa sababu licha ya juhudi za dhati za watu wengi na majadiliano yaliyopiga hatua hakuna matokeo yaliyopatikana wakati wa majadiliano haya. Pia ninasikitika kwamba mchakato mzima ulikuwa wa fujo ingawa pia hili linapaswa kuwa funzo”
Umoja wa Ulaya na China wato wito wa hatua za mabadiliko ya tabia nchi kuchukuliwa
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wamezilalamikia nchi wazalishaji wa mafuta kama kizingiti cha mafanikio ya rasimu hii kutokana na maslahi ya kiuchumi. Florian Titze kutoka Taasisi ya Mazingira WWF nchini Ujerumani amesema kuwa ni bora kutokuwa na makubaliano kabisa badala ya kukubali mkataba usiosaidia lolote kutatua tatizo la plastiki duniani.
Naye mjumbe wa Colombia Haendel Rodriguez amesema rasimu hii imezuiwa na kundi dogo la nchi ambazo hazikutaka kufikiwa kwa makubaliano hayo. Kutokana na hali hii wadadisi wa mazingira wanasema haijulikani mstakabari wa juhudi za kukomesha tatizo la plastic ulimwenguni.