Makubaliano ya kihistoria ya kibiashara kati ya Ujerumani na Rashia
12 Aprili 2005Hannover:
Ujerumani na Rashia zimedhamiria kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.Wanaviwanda wa nchi hizi mbili wamekubaliana juu ya miradi itakayogharimu mabilioni ya Euro katika sekta ya usafiri na nishati.Jumla ya mikataba minane imetiwa saini katika sherehe maalum katika uwanja wa maonyesho ya kimataifa mjini Hannover.Kampuni la BASF litakua la kwanza la kigeni kushiriki katika mradi wa kuchimba na kusambaza gesi nchini Rashia.Kwa upande wake kampuni kubwa kabisa la gesi la Rashia Gasprom litaruhusiwa kuuza nishati hiyo barani Ulaya.Rais Vladimir Putin wa Rashia na kansela Gerhard Schröder wamezungumzia juu ya hatua ya kihistoria kati ya nchi hizi mbili.Nalo kampuni la Siemens na shirika la reli la Rashia yametiliana saini mkataba wa euro bilioni moja kwaajili ya ujenzi wa treni 60 za mwendo wa kazi.Ushirikiano wa dhati kati ya Ujerumani na Rashia unatazamiwa pia kutuwama katika sekta ya elimu na utafiti.