Riek Machar aishutumu Uganda kwa kukiuka marufuku ya silaha
25 Machi 2025Katika barua yake aliyoituma kwenda kwa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo na Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika, IGAD, Machar amesema uvamizi wa jeshi la Uganda nchini Sudan Kusini, umekiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2018, ambayo yalivimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.
Uganda ilisema ilipeleka wanajeshi wake Sudan Kusini mapema mwezi huu, kutokana na kuvunjika kwa uhusiano wenye uhasama kati ya Machar na Rais Salva Kiir.
Barua hiyo iliyoandikwa na Machar, Machi, 23, imeeleza kuwa vikosi vya Uganda kwa sasa vinafanya mashambulizi ya anga dhidi ya raia, akihimiza Uganda iwekewe shinikizo la kuwaondoa wanajeshi wake. Msemaji wa ofisi ya Machar, amethibitisha ukweli wa barua hiyo iliyoonekana na shirika la habari la Reuters.
Uganda yaidhinisha kupelekwa wanajeshi
Hata hivyo, wasemaji wa majeshi ya Uganda na Sudan Kusini hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa marufuku ya silaha iliyowekwa tangu Julai, 2018.
Wiki iliyopita, bunge la Uganda liliidhinisha kupelekwa wanajeshi Sudan Kusini. Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Jacob Markson Oboth alisema kuwa kupelekwa kwa wanajeshi hao kulikuwa na lengo la kuzuia janga la kiusalama katika taifa hilo.
Uganda inahofia kuzuka kwa ghasia kali katika nchi hiyo jirani inayozalisha mafuta, zinaweza kuchangia wimbi la wakimbizi kuvuka mpaka na kusababisha kukosekana kwa utulivu.
Mwanzoni mwa mwezi Machi, vikosi vya usalama viliwakamata washirika kadhaa wakuu wa Machar, kufuatia mapigano katika eneo la kaskazini mashariki kati ya jeshi na wanamgambo wa kikabila wa White Army, ambao serikali inawashutumu kwa kumuunga mkono Machar.
Ingawa vilipigana pamoja dhidi ya vikosi vya Kiir wakati wa mzozo wa 2013 hadi 2018, chama cha Machar cha SPLM-IO kinakanusha kuwa na mafungamano yoyote na White Army.
Umoja wa Mataifa waonya hatari ya Sudan Kusini kurudi vitani
Aidha, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan Kusini, Nicholas Haysom, ameonya kuwa kuongezeka kwa matamshi ya chuki kunaweza kuirudisha tena nchi hiyo kwenye mzozo wa kikabila.
"Hali ya kisiasa na kiusalama inazorota kwa kiasi kikubwa, tangu White Army walipovamia kambi ambazo awali zilikuwa zinakaliwa na vikosi vya ulinzi vya Sudan Kusini huko Nashir, Machi 4. Mashambulizi haya holela dhidi ya raia yanasababisha hasara kubwa na majeraha ya kutisha, ikiwemo kwa wanawake na watoto," alifafanua Haysom.
Wakati huo huo, msemaji wa vikosi vya SPLM-IO, Lam Paul Gabriel, amesema moja ya kambi zake za jeshi karibu na mji mkuu, Juba, ilishambuliwa Jumatatu usiku, huku Marekani ikionya kwamba ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa ghasia kati ya makundi mawili hasimu.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini hakupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo.
(AFP, Reuters)