Makadinali wa Kanisa Katoliki kuendelea kumchagua Papa Mpya
8 Mei 2025Hayo ni baada ya zoezi hilo kutofaulu usiku wa Jumatano na asubuhi ya Alhamisi na ndipo dohani ya kanisa hilo dogo ilitoa moshi mweusi kama ishara kwamba Papa mpya hajapatikana. Maelfu ya watu wamekusanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro kusubiri kuuona moshi huo.
Katika miaka ya hivi karibuni, hakuna Papa aliyechaguliwa katika duru ya kwanza, hivyo moshi mweusi wa jana na leo asubuhi ulitarajiwa, lakini kwa kuzingatia historia, matokeo ya mwisho huenda yakapatikana katika siku ya pili ya upigaji kura. Hata hivyo hadi duru nne za upigaji kura zinaweza kufanyika kabla ya Papa mpya kuchaguliwa.
Papa Mpya anahitaji kupata theluthi mbili ya kura za Makadinali au kukusanya jumla ya kura 89 katika zoezi hilo linalofanyika kwa faragha. Moshi mweupe ndio huashiria kama Papa Mpya amepatikana.