Makadinali bado kumchaguwa Papa mpya.
19 Aprili 2005Moshi mweusi umeonekana juu ya chumba cha Sixtine leo mchana na alaasiri,kama dalili kwamba bado Papa kupatikana.Uchaguzi utaendelea kukiwa na mategemeo kuwa makadinali watakuwa wamekwishakubaliana kuhusu mtu mmoja mnamo siku mbili zijazo.
Hadi wakati huu bado hakuna makubaliano kuhusu Papa mpya baada ya kura mbili za alaasiri.Kunasubiriwa matokeo ya kura zingine mbili zinazosalia kwa leo ambayo yanatarajiwa kutangazwa saa 1 jioni.
Wakati wa mchana kulikuwa kumefanyika kura zingine mbili ambazo matokeo yametatanisha kidogo.Radio Vatican imehakikisha kuwa moshi uliotolewa kupitia shemini ulikuwa mweusi.Wakati huo hali ya sintohafamu ilikuwa imetawala miongoni mwa mashahidi ambao kwa maoni yao,mara moshi ulikuwa mweusi,mara nyingine wenye rangi nyingine.Kwa vyovyote vile hafifu.
Hakikisho jingine kwamba bado hatua kupigwa,ni kengele za minara ya Vatican ambazo zimesalia kimya.Imepangwa kuwa zitalia kote Vatican na Roma endapo Papa atapatikana.
Muda mfupi baada ya moshi huo wa mara ya kwanza kwa leo,kumeonekana moshi mungine daima mweusi lakini safari hii kengele za kanisa kuu la Mtakatifu Peter zimelia.Watu wamezidi kuchanganyikiwa kufuatia matukio hayo.
Hakuna maelezo yoyote yale yaliotolewa kuhusu hatua hiyo ya pili ambayo wadadisi wa mambo wanahisi imefanywa kwa lengo la kukomesha shaka shaka kuhusu rangi ya moshi wa mara ya kwanza.Moshi wa mara ya pili umeambatana na milio ya minara ya Vatican ambayo ilikuwa ikitangaza majira ya saa sita adhuhuri.
Kwa hiyo hadi sasa zimeshafanyika kura nne bila mafanikio.Kumekuwa na tetesi kwamba huenda Papa mpya kapatikana leo au kesho,lakini hayo ni mategemeo ya watu tu.
Kulingana na utaratibu mzima wa kumchagua Baba wa kanisa la kikatoliki duniani,kunafanyika kura mara mbili asubuhi na mara mbili vile vile alaasiri.
Matokeo ya kura mbili yanaunguzwa kwa pamoja na kutoa moshi mweusi kama hakuna maridhiano na moshi mweupe kama wamekubaliana.Wakati huo minara yote italia.Na Televisheni ya Vatican ambayo inaonyesha moja kwa moja duniani kote moshi huo,itawaalika pia waumini kufika uwanja wa Mtakatifu Peter ambako Papa mpya bila shaka atajitokeza kwa hotuba fupi.
Ili achaguliwe,itabidi apate ang’alau theluthi mbili za kura yaani 77 miongoni mwa kura 115 za makadinali wanaoshiriki katika zoezi hilo.
Maelfu kadhaa ya waumini wamekusanyika nyakati za adhuhuri uwanja wa St Peter’s kushuhudia matokeo ya kura za asubuhi.Baadhi yao wakiwa tayari kupiga picha.Jana katika siku ya kwanza ya mkutano,watu walikuwa wengi mno.
Wachunguzi wa mambo ya Vatican wanahisi kuwa katika uchaguzi huo usiyofanyiwa kampeni wala wagombea kujitokeza,kura za jana zilisaidia kambi mbili kupima nguvu.Kambi ya kwanza ni yile yenye makadinali wenye nadharia kali.Ya pili inaundwa na makadinali wanaopendelea mageuzi.
Huenda kura za pande hizo zilikwenda kwa Kadinali kutoka Ujerumani Joseph Ratsinger na Kadinali kutoka Milan Carlo Maria Martini.Lakini daima kulingana na wadadisi wa mambo ya Vatican,huenda kukachaguliwa mtu mungine wa msimamo wa kadiri.Pia kura za jana huenda zikawa zilisaidia kudhihirisha makadinali wenye usemi mkubwa,wanaoweza kuwaelekeza wengine kwa njia moja ama nyingine.
Ikiwa Papa mpya hatopatikana mnamo siku tatu za mkutano yaani hadi jana jioni,basi makadinali watapumzika siku moja ya kutafakari,kabla ya kuendelea.
Tangu mwanzoni mwa karne iliopita,hakuna mkutano wa kumchagua Papa uliozidisha siku tano.Marehemu Papa Yohana Paulo wa II ambae alifariki dunia mwanzoni mwa mwezi huu,aliteuliwa katika siku ya tatu.Mtangulizi wake Yohana Paulo wa kwanza katika siku ya pili.