Makabiliano zaidi ya 100 na Urusi yaripotiwa Ukraine
21 Julai 2025Matangazo
Urusi inaendelea mbele na operesheni yake ya kijeshi mashariki mwa Ukraine huku yakiripotiwa makabiliano zaidi ya 100 yaliyotokea siku moja jana Jumapili.
Mnadhimu wa jeshi mjini Kiev amesema mashambulizi 122 ya Urusi yaliripotiwa kutwa nzima hapo jana. Wakati wa mashambulizi ya kutokea angani, mabomu 71 yalidondoshwa katika maeneo ya Ukraine, ingawa takwimu hizo hazikuweza kuthibitishwa kwa njia huru.
Jeshi limesema mapigano makali yalitokea katika viunga vya mji unaozozaniwa wa Pokrovsk, huku vikosi vya Urusi vikifanya mashambulizi 36 huko kutokea pande tofauti.
Pokrovsk ni mji muhimu kimkakati kwa ajili ya usafiri magharibi wa eneo la Donetsk ambao umekuwa ukishuhudia mapigano kwa miezi kadhaa na umekaribia kuharibiwa kabisa.