Mazungumzo ya kunusuru usitishaji vita Gaza yapiga hatua
13 Februari 2025Juhudi za kuyaokoa makubaliano hayo zinalenga pia katika kuhakikisha kuwa pande hizo mbili zinabadilishana wafungwa kwa mateka mwishoni mwa juma kama ilivyopangwa.
Chanzo kimoja kilicho karibu na mazungumzo hayo ya kuyaokoa makubaliano ya Hamas na Israel, kimesema kuwa wasuluhishi wamefanikiwa kupata ahadi ya Israel ya kuzingatia misingi ya kiutu kuanzia Alhamisi asubuhi.
Chanzo kingine kutoka upande wa Palestina kimesema kundi la Hamas limethibitisha kwa maafisa wa Misri kuwa litafanya awamu ya sita ya kubadilishana wafungwa kwa mateka kwa wakati ifikapo Jumamosi mara tu Israel itakapotimiza wajibu wake katika makubaliano yao.
Soma zaidi: Wapatanishi wapambana kunusuru makubaliano ya Gaza
Taarifa kutoka katika chanzo cha kwanza imesema kuwa mara tu wasuluhishi watakapothibitisha idhini ya mwisho ya Israel, vifaa kama vile mahema mafuta, dawa, na vifaa vya kukarabati hospitali na kila kinachohusika na misingi ya kiutu kinaanza kuingia katika Ukanda wa Gaza.
Makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas, yamekuwa katika hatihati ya kuvunjika katika siku za hivi karibuni baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuonya kuwa mambo yatakuwa mabaya kwa wanamgambo wa Hamas kama watashindwa kuwaachilia mateka wote ifikapo Jumamosi.
Kundi la Hamas, liliituhumu Israel kwa kushindwa kutimiza baadhi ya masharti chini ya makubaliano ya kusitisha vita ikiwemo kushindwa kupeleka vifaa muhimu kama vile mahema na misaada mingine na kutishia kuwa wangechelewesha kuwaachilia mateka katika awamu ijayo. Kundi hilo hata hivyo limesisitiza kuwa halitaki makubaliano ya kusitisha vita yavunjike.
Matumaini licha ya makubaliano ya kusitisha vita kuwa hatarini
Licha ya tishio la kuvunjika kwa makubaliano kati ya pande hizo mbili baadhi ya wakaazi wa Gaza wameonesha matumaini kuwa huenda pande hizo zikamaliza tofauti zao na kuendelea kubadilishana mateka na wafungwa.
Mmoja wa wakaazi hao Abdul-Nasser Abu al-Omrain amesema kuwa, ''Kwa maoni yangu vita havitaendelea kwa sababu hakuna mwenye nia ya kurejea vitani. Si Hamas wala Israel wanaotaka kurudi kwenye mapigano. Vita vina madhara kwa pande zote zinazohusika.''
Kwingineko Mashariki ya Kati, gazeti la Washington Post la Marekani lililochapishwa Jumatano limesema taarifa za kiitelijensia za Marekani zimetoa tahadhari kuwa huenda Israel ikafanya shambulio dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran ifikapo katikati mwa mwaka huu.
Gazeti hilo limesema serikali ya Israel, Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA na ofisi ya Mkurugenzi wa Intelijensia wa Marekani h wamekataa kuzungumza lolote kuhusu taarifa hizo .
Hata hivyo, msemaji wa ikulu ya Marekani Brian Hughes, ameliambia gazeti hilo kuwa rais Donald Trump hatoruhusu Iran iwe na silaha za nyuklia.