Maisha ya kawaida yarudi mpakani Uganda na DRC
1 Agosti 2025Maisha yanarejea taratibu katika hali ya kawaida kwenye maeneo ya mpakani kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yanayodhibitiwa na waasi wa M23, kufuatia kufunguliwa tena kwa vituo viwili vya mpakani vya Bunagana na Ishasa. Vituo hivi vilikuwa vimefungwa tangu Juni 2022, wakati waasi walipoliteka eneo hilo.
Kulikuwa na shamrashamra katika mji wa Bunagana, ulioko Wilaya ya Kisoro kusini magharibi mwa Uganda, pamoja na upande wa pili wa mpaka ndani ya DRC, wakati Mkuu wa Wilaya ya Kisoro, Hajji Badru Sebyala, alipoongoza hafla ya kufungua tena mpaka tarehe 10 Julai 2025. Tukio hilo lilifanyika chini ya ulinzi mkali.
"Tunashukuru serikali ya Uganda kwa uamuzi wake wa kufungua tena mpaka huu. Tulikuwa tunakabiliwa na mgogoro mbaya wa kiuchumi,” alisema mkazi mmoja wa Bunagana aliyezungumza na DW, akieleza furaha yake kuona malori ya mizigo yakivuka tena mpaka yakiwa yamesheheni bidhaa.
Ahueni yake ilielezewa pia na wenzake wengi katika eneo hilo, ambao walikuwa wametaabika kwa miaka mitatu ya kufungwa kabisa kwa mpaka huo. Malori na mabasi yaliyokuwa yakihudumu kati ya Bunagana na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, yalikuwa yamesitisha shughuli, na hivyo kukata njia muhimu ya kiuchumi. Kufungwa huko kulilemaza biashara ya ndani, kuanzia kazi ndogo ndogo kama kubeba mizigo na usafiri wa bodaboda hadi huduma za mapokezi.
Mtoto wa Rais Museveni alishawishi mchakato huo
Wakati akipongeza uamuzi wa kufungua tena vituo vya mpakani, Mku wa Wilaya ya Kisoro, Abel Bizimana, alisisitiza wito wake kwa viongozi wa kisiasa wa nchi tatu za Uganda, Rwanda na DRC kutambua kuwa "uhusiano wa kikabila wa eneo hili ndio chanzo cha mshikamano miongoni mwa jamii zilizogawanywa na mipaka ya kikoloni.”
Kabla ya kufunguliwa kwa mipaka ya Bunagana na Ishasha, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Uganda na mwana wa Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni, alikuwa ameandika ujumbe kwenye akaunti yake ya X, akihoji busara ya kiongozi yeyote kuendelea ''kuwatenganisha watu wamoja kidamu na kimila kwa muda mrefu.''
Uganda iliamua kufunga mpaka baada ya serikali ya Congo kusema kuwa kundi la waasi la M23 lilikuwa likinufaika pakubwa na ushuru uliokuwa unakusanywa katika maeneo hayo, na hivyo kusaidia kufadhili shughuli zao za kivita.
Kwa baadhi ya watu hilo lilituma ujumbe kwamba yumkini Uganda ilikuwa ikiunga mkono shughuli za M23 chini kwa chini. Ili kuondoa dhana hiyo, mipaka ilifungwa—ingawa Uganda tayari ilikuwa imeanzisha mradi wa kujenga barabara za kuingia ndani ya DRC kwa lengo la kuimarisha biashara baina ya mataifa hayo mawili.
Katika kipindi hicho, biashara pande zote mbili ziliathirika, kwani malori ya mizigo kutoka Kenya na nchi nyingine hayakuweza tena kupita katika njia hiyo muhimu.
Jamii ya wapenda amani iliyojikuta katikati ya vita visivyokwisha vya raslimali
Ukitembea katika masoko ya Bunagana, upande wa DRC, unakutana na watu wapenda amani ambao hawana chaguo jingine bali kuukubali utawala wa waasi wa M23. Kwa hofu ya kulipiziwa kisasi, hakuna yeyote aliyekuwa tayari kuzungumza wazi na vyombo vya habari.
Kuna hofu kubwa kuwa serikali ya Kinshasa ina wapelelezi waliopenyezwa katika jamii, jambo linalowafanya wengi kutozungumza kwa uhuru lolote linalohusiana na siasa. Katika muktadha huu, alipoulizwa na DW, Mkuu wa Mji wa Bunagana, Désiré Kanyamarere, alishauri maswali yote yaelekezwe kwa msemaji wa M23 aliyeko mjini Goma.
Kufungwa kwa mpaka kwa miaka mitatu kuligeuza Bunagana kuwa mji uliosinzia, huku majengo mengi ya biashara yakiwa yamefungwa na wamiliki wa nyumba wakikabiliwa na madeni makubwa na mikopo ya benki wasiyoweza kuilipa.
Mfanyabiashara mmoja kutoka Bunagana, Idriss Uwanjye, aliambia DW kuwa wakati wa kufungwa kwa mpaka, ilikuwa inawezekana kusafirisha bidhaa kwa njia ya magendo—japo haikuwa kazi rahisi hata kidogo.
"Ili kusafirisha bidhaa kuvuka mpaka, mtu alilazimika kulipa ada zisizo rasmi kwa waasi wa M23,” Uwanjye alieleza siku ya kufunguliwa kwa mpaka. "Kiasi kilikuwa kikiamuliwa na afisa wa waasi bila vigezo vyovyote, jambo lililofanya iwe vigumu kujua la kutarajia.”
Serikali ya DRC haikufurahishwa na uamuzi wa Uganda
Vyanzo kutoka upande wa Congo vinaeleza kuwa hakukuwa na mashauriano yoyote na Kinshasa kabla ya Uganda kufanya uamuzi wa upande mmoja wa kufungua tena mipaka ya Bunagana na Ishasha.
Siku mbili baada ya kufunguliwa, Gavana wa Kivu Kaskazini, Jenerali Évariste Kakule Somo, alimwita Balozi Mdogo wa Uganda Isingoma Isimererwa, kwa mazungumzo mjini Beni, mji ambao hivi sasa ni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini baada ya Goma kutekwa na waasi wa M23.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Balozi Isimererwa alitoa wito wa utulivu na subira, akisema kuwa taarifa rasmi ingetolewa na serikali ya Uganda.
Nafasi ya Uganda katika mzozo huu inasalia kuwa tata. Kwa upande mmoja, inashukiwa kuisaidia M23; kwa upande mwingine, inashirikiana na serikali ya Kinshasa katika operesheni za kijeshi za pamoja dhidi ya waasi wa ADF, kundi la waasi wa Uganda linalondesha harakati zake katika mkoa wa Ituri mashariki mwa Congo.
Maslahi ya kiuchumi ya Uganda huenda ndiyo sababu ya kufunguliwa kwa mpaka?
Kwa ujumla, kiwango cha biashara kati ya Uganda na DRC kilipungua kwa kiasi kikubwa, huku kituo cha Rubavu kati ya Rwanda na DRC kikishuhudia ongezeko kubwa la shughuli za biashara na usafirishaji. Malori mengi na biashara kutoka Afrika Mashariki yalibadilisha njia na kuelekea Rubavu, hali iliyoufanya mji huo pacha na Goma kuwa mojawapo ya vituo vya mpakani vyenye shughuli nyingi zaidi barani Afrika.
Abel Bizimana, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kisoro, alieleza kuwa ana imani katika ushirikiano na utawala wa waasi wa M23. "Tulipofungua tena mpaka, wawakilishi wa M23 walinihakikishia kuwa usalama utadumishwa—kwa mpaka wenyewe, kwa mizigo, na kwa watu,” alisema Bizimana, akithibitisha kuwa Uganda sasa inawatambua waasi hao kama utawala mbadala katika maeneo wanayoyadhibiti.
Je, Uganda ilitambua kuwa ilikuwa ikipoteza fursa za kiuchumi kwa Rwanda? Licha ya tishio la mashambulizi ya waasi wa M23, biashara mjini Goma—kitovu cha biashara cha mashariki mwa DRC—iliendelea kustawi. Ustahimilivu huu uliendelea hata baada ya kundi hilo la waasi kuuteka mji huo Januari 2025 na kuimarisha mamlaka yake.
Wakati DRC ikiendelea kuishutumu vikali Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma hizo mara kwa mara. Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais wa Rwanda Paul Kagame alielekeza lawama kwa Uganda, akidai kuwa M23 walianzisha mashambulizi yao kutoka ardhi ya Uganda, sio Rwanda.