Mahujaji wa kiislamu wawasili Makka kwa ibada ya Hijja
2 Juni 2025Saudi Arabia imechukua hatua madhubuti kukabiliana na athari za joto kali wakati wa ibada ya Hija, kufuatia maafa ya mwaka jana ambapo mahujaji 1,301 walifariki kutokana na joto lililofikia hadi nyuzi joto 51.8°C. Mwaka huu, zaidi ya mashirika 40 ya serikali na takriban maafisa 250,000 wanahusika katika maandalizi ya kuhakikisha usalama na ustawi wa mahujaji. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza maeneo yenye kivuli, kuongeza idadi ya wahudumu wa afya, na kutumia mbinu maalum za kupunguza athari za joto kali.
Idadi ya mahujaji waliofariki yaongezeka na kufikia zaidi ya watu 1,300
Teknolojia ya kisasa, hasa ya akili mnemba (AI), itatumika kwa kiwango kikubwa kusimamia idadi kubwa ya mahujaji. Mamlaka pia zimeanzisha misako dhidi ya mahujaji wasiosajiliwa kwa kutumia droni, huku ujumbe wa tahadhari ukitumwa kupitia simu za mkononi ili kutoa taarifa kwa haraka.
Kwa mujibu wa Hammoud Al-Faraj, Mkurugenzi Mkuu wa Ulinzi wa Raia, juhudi zinaendelea kuimarisha mifumo ya usalama na ufuatiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kuhakikisha ibada ya Hija ya mwaka huu inafanyika kwa usalama na utulivu zaidi.
Saudia: Atakaeingia Makka bila kibali wakati wa Hijja atakamatwa
Wakati maandalizi ya ibada ya Hija yakifikia kilele, mamlaka za Saudi Arabia zimeripoti kuwa hadi sasa, zaidi ya watu 270,000 wamezuiwa kuingia mjini Makka kwa kukosa vibali rasmi. Vilevile, zaidi ya kampuni 400 zisizoidhinishwa zimebainika, pamoja na magari 5,000 yaliyokuwa yakisafirisha mahujaji kinyume cha sheria.
Leseni za Hija hutolewa kwa mfumo maalum wa mgao kwa kila nchi, na baadaye hugawiwa kwa watu binafsi kupitia bahati nasibu. Hata hivyo, gharama kubwa za safari hii takatifu huwafanya baadhi ya watu kujaribu kutekeleza ibada ya Hija bila vibali halali, bila kujali hatua kali za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Mahujaji wa Kiislamu wajiandaa kwa ibada rasmi ya Hija
Kwa mujibu wa mamlaka, mtu yeyote atakayepatikana akiingia Makka bila kibali wakati wa Hija atakabiliwa na faini kubwa, kukamatwa, kufukuzwa nchini, na huenda akapigwa marufuku ya kuingia Saudi Arabia kwa hadi miaka 10.
Ibada ya Hija ya mwaka huu inatarajiwa kuanza siku ya Jumatano, huku takriban mahujaji milioni 1.5 wakitarajiwa kushiriki. Hii ni idadi ndogo ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo mahujaji walifikia milioni 1.8.
Hija ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu na ni tukio kubwa la kidini linaloipa Saudi Arabia hadhi ya kiroho na ya kimataifa. Mbali na umuhimu wake wa kiimani, ibada ya Hija pia ni chanzo kikubwa cha mapato ya uchumi, kupitia huduma na miundombinu ya kuwahudumia mahujaji kutoka duniani kote.
afp/ap